KAMPUNI
ya Acacia Mining PLC imesema itailipa serikali kodi ya dola za
Kimarekani milioni 20 mwaka huu baada ya kusainiwa mkataba wa maridhiano
kati yake na Mamlaka ya Mapato (TRA) mwezi uliopita jijini Dar es
Salaam.
Makubaliano
hayo baina ya Acacia na TRA ni kilele cha mchakato uliofanywa kwa lengo
la kuendeleza dhamira ya utendaji ya kampuni hiyo nchini Tanzania na
kuongeza ushirikiano na wadau mbalimbali wa kampuni hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bradley Gordon, alitoa taarifa hiyo kwenye mawasiliano na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema
kutokana na makadirio, kampuni hiyo italipa kodi ya ushirika ya miaka
mitatu, endapo kampuni hiyo mwaka huu itaingiza mapato yanayofikia kiasi
cha dola za Marekani milioni 80.
Alisema
mkataba kati ya Acacia na TRA umetiwa saini na umetambuliwa na pande
zote mbili kwamba hakuna kodi yoyote ya mapato yatokanayo na faida
ambayo Acacia inastahili kulipa, haitalipwa.
Gordon
alisema Acacia Mining ambayo iliingia nchini katika sekta ya madini
ikijulikana kama Barrick na baadaye kama African Barrick Gold miaka 15
iliyopita, imekuwa ikitengeneza faida lakini haijarejesha mtaji
iliowekeza wa dola za Kimarekani bilioni 3.8.
Hivi
karibuni, Baraza la Rufaa za Kodi (TRAT), liliamua katika rufaa
iliyokatwa na Acacia kwamba kampuni hiyo ilijenga mazingira ya kukwepa
kodi ya dola za Marekani 41,250,426 (Sh bilioni 89) kwa kipindi cha
miaka minne mfululizo.
Katika
hukumu hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa TRAT, Jaji Dk Fauz Twaib,
ilielezwa kuwa fedha hizo zilizopaswa kulipwa na ABG kwa TRA kama kodi
ya zuio katika kipindi hicho, lakini ikakata rufaa kupinga kodi hiyo na
baraza hilo kuipa haki TRA.
Hata
hivyo, Acacia imepinga uamuzi huo katika Mahakama ya Rufaa.
Akizungumzia historia ya mgodi huo, Gordon alisema wakati Barrick
ilipoingia Tanzania miaka zaidi ya 15 iliyopita, kulikuwa na shughuli za
kiwango kidogo za migodi nchini.
Gordon
alisema tangu wakati huo, Barrick, African Barrick Gold na kisha Acacia
Mining zimewekeza kiasi cha dola bilioni 3.8 katika ujenzi na
uendelezaji wa migodi mitatu iliyopo hadi sasa.
Alisema
Tanzania sasa ni mzalishaji mkuu wa nne wa dhahabu duniani, na kwamba
kampuni yao ndiyo wazalishaji wakubwa nchini jambo alilosema hawana budi
kujivunia.
Akizungumza
madai kwamba wanatoa taarifa za uongo za kupata hasara ili kukwepa
kulipa kodi nchini , alisema akaunti zao pamoja na zile za migodi
mingine duniani hufanyiwa uhakiki makini.
“Kwa
Tanzania peke yake, kuna mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Shirika
la Uhakiki wa Migodi, Mahakama ya Udhibiti na Mamlaka ya Mapato Tanzania
–taasisi zote hizi zinapembua hesabu zetu.
"Kwa kuwa tuna Soko la Hisa la London lenye umahiri mkubwa nalo pia linafanya kazi makini kuhakiki shughuli zetu,” alisema.
Alisisitiza
kuwa hawajakwepa kulipa kodi bali katika biashara, panahitajika kwanza
kuondoa gharama zote katika mapato kabla ya kutangaza kwamba wamepata
faida.
Alisema
katika miaka sita iliyopita pekee, tumelipa zaidi ya dola za Kimarekani
milioni 750 kama kodi na mrabaha nchini Tanzania, karibu mara mbili ya
kiasi ambacho wanahisa wamepokea kama mgao.
Gordon
alisema wamewekeza dola za Kimarekani milioni 65 kwenye miradi ya
maendeleo ya jamii . Alisema hivi sasa wanatoa ajira zaidi ya 45,000
nchini.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment