Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Awakomalia Washtakiwa wa Tumbili ...Mawakili wa Washtakiwa Wapambana Ili Wateja Wao Wapatiwe Dhamana

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha mahakamani hati ya kupinga dhamana kwa washtakiwa wa kesi ya kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Armenia.
Hata hivyo, jopo la mawakili watano wa utetezi wakiongozwa na wakili maarufu kutoka jijini Dar es Salaam, Majura Magafu, walipinga hati hiyo wakidai haijawasilishwa kihalali mahakamani.

Hati hiyo iliwasilishwa Mahakama Kuu Moshi jana na mawakili wa Serikali, Wancho Simon na Salim Msemo, muda mfupi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa maombi ya dhamana ya washtakiwa hao.

Akiwasilisha pingamizi la hati hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari, Wakili Magafu alisema DPP alipaswa kuwasilisha hati tatu tofauti kwa kila maombi badala ya kuwasilisha hati moja.
“Hati hii iliwasilishwa kabla ya amri ya Mahakama yako ya kuyaunganisha maombi ya dhamana ya washtakiwa, kwa hiyo DPP alipaswa kuwasilisha hati kulingana na kila maombi,” alidai Magafu.

Alisema maombi yao ya dhamana yamesajiliwa kwa namba 3/2016, 4/2016 na 5/2016, DPP alitakiwa kuwasilisha hati tatu tofauti kwa maana ya hati moja kwa kila maombi yaliyoko kortini.
“Hoja yetu hapa ni je hati hii ya DPP iko sahihi mbele ya Mahakama yako? Ombi letu ni uitupilie mbali na ombi letu la dhamana lisikilizwe,” aliomba Magafu.

Hata hivyo, wakili huyo alisema kama Mahakama itaona hati hiyo imewasilishwa kihalali, basi iwaruhusu kuzungumzia uhalali wa hati yenyewe kisheria na madhara yake.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Simon alisema wakili mwenzake (Magafu) anaipotosha Mahakama na hakunukuu sheria yoyote inayoipa nguvu hoja yake ya kupinga hati hiyo ya DPP.

Wakili huyo alifafanua, hata hati za kuitwa shaurini walizotumiwa hazikuwa tofauti kulingana na namba za maombi, bali walitumiwa hati moja ikitaja maombi yote sehemu moja.

Akitoa uamuzi mdogo kuhusu mabishano hayo, Jaji Sumari alisema amepitia kwa umakini hati ya DPP na kujiridhisha kuwa iko sahihi mbele ya Mahakama.
Hata hivyo, Jaji Sumari alisema hoja ya hati hiyo imewasilishwa kabla ya wakati na kuutaka upande wa mashtaka kuwasilisha kwanza kiapo kinzani leo.

Alisema kama mawakili wa utetezi watakuwa na majibu ya ziada kutokana na kiapo hicho kinzani, wawasilishe majibu kesho na majibizano yasikilizwe Aprili 14, mwaka huu.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment