Ikiwa
ni takriban miezi mitano tangu kutoka madarakani, Rais wa awamu ya nne,
Jakaya Kikwete, amesema kwa sasa anafurahia maisha ya uhuru baada ya
kustaafu kwake na kwamba anajiandaa kuwa mzee mashuhuri nchini
atakapokabidhi chama.
Kikwete
alistaafu rasmi Novemba 5, mwaka jana baada ya kuapishwa kwa Rais wa
awamu ya tano, Dk. John Magufuli, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa
Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Juni, mwaka huu.
Akihojiwa
na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Kikwete alisema maisha nje ya Ikulu ya
Magogoni, ni mazuri kwa sababu ametua mzigo wa kuhudumia watu milioni 50
na kwamba sasa anaendelea na mambo yake binafsi.
“Maisha
baada ya kutoka madarakani, ni mazuri kwa sababu sina presha niliyokuwa
nayo, nilikuwa na mzigo mkubwa wa kuangalia taifa hili la watu milioni
50, siyo mzigo mdogo, ni kazi kubwa, una hili, una hili unarudi
nyumbani…
“Sasa
hivi unarudi nyumbani hauna faili, ninafanya mambo ninayoyapanga mimi,
na shughuli ninazofanya ni za kimataifa tu, niko kwenye hili la Libya
(mjumbe wa usuluhishi wa mgogoro wa Libya), naondoka karibuni, tuna
mkutano Marekani wa mambo ya malaria.
“Nipo
kwenye Kamisheni ya Elimu na Waziri mkuu Gordon Brown, (Waziri Mkuu wa
zamani wa Uingereza), pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
nafanya shughuli nyingi tu sasa hivi," alisema na kuongeza:
“Kuhusu
siasa, bado ni Mwenyekiti wa CCM na baada ya muda, nitakabidhi (chama)
baada ya hapo kila kitu nitamuachia mzee Magufuli aendelee nayo, mimi
nitabaki ni mzee tu maarufu katika nchi yetu, maisha ni mazuri tu."
Novemba,
mwaka jana, baada ya kutoka madarakani, Kikwete kwa mara ya kwanza
alionekana eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam alipokwenda kufanya
manunuzi na mkewe Salma.
Baadhi
ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Kikwete alikuwa amevalia suti
maarufu kama ‘kaunda suti’ ya rangi nyeusi, alionekana akiingia katika
viunga vya Mlimani City saa 5:00 asubuhi.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema Kikwete aliwasili katika maeneo hayo akiwa katika msafara wa magari manne na pikipiki moja.
Hatua hiyo ilionekana kushangaza baadhi ya watu waliokuwapo katika maeneo hayo, huku wengi wao wakionekana kutaka kumsalimia.
Akiwa
kwenye eneo hilo, Kikwete na mkewe, waliingia katika maduka ya Game na
kufanya manunuzi kwa dakika zisizopungua 10 hadi 15 na baadaye kutoka
nje na walinzi wake wakionekana kubeba mifuko iliyokuwa na bidhaa
walizonunua.
Kama
ilivyo hulka ya Rais Kikwete, alipotoka nje ya duka hilo, alianza
kusalimiana na mtu mmoja ambaye alionekana kufahamiana naye.
Hatua hiyo ilimpa fursa ya kuwasalimia watu wengine waliokuwa karibu na tawi la benki moja.
Baada ya hapo, msafara wake uliondoka na kuelekea barabara ya Sam Nujoma.
Tangu
achaguliwe kuwa Rais mwaka 2005, itifaki na majukumu yake ya urais,
yalikuwa yakimbana Rais Kikwete na hivyo kushindwa mambo yake binafsi
kama walivyo raia wengine.
Aidha,
tangu alipoachia kiti cha urais na kumkabidhi Dk. Magufuli baada ya
kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, Kikwete amekuwa akiishi nyumbani kwake
Msoga mkoani Pwani na mara chache amekuwa akienda Ikulu kuteta na Rais
Magufuli.
Kikwete aliondoka rasmi Ikulu na familia yake Novemba 6, mwaka jana na kuanza maisha mapya kijijini kwake Msoga.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment