Hata hivyo, mara tu aliposhikwa usingizi, simu yake ya mkononi ikalia. Ilikuwa kunako saa nne na nusu Jumamosi ya tarehe 6. Madaktari walimpigia simu arejee hospitalini kwa vile hali yangu ilikuwa imezidi kuwa mbaya.
ENDELEA…
Wakati huo nilikuwa katika kitengo cha HDU kwa muda ambao haukufika hata saa mbili. Akikumbukia hali ambayo aliniacha, mara moja alimchukua mkewe na kuharakisha kuja hospitalini.
Madaktari walimwambia hali yangu ilikuwa imezorota sana. Walikuwa wamefanya kila waliloweza lakini nilikuwa sionyeshi hali ya kutambua chochote.
Baada ya majadiliano mafupi waliamua nihamishiwe katika kitengo cha wagonjwa mahututi ambacho nchini Uingereza huitwa Intensive Therapy Unit (ITU) na nchi zingine huita Intensive Care Unit (ICU).
Nikiwa humo, niliwekewa mashine nyingi za kunifanyia uchunguzi na madaktari walichomeka mipira katika kila upenyo wa mwili wangu kwa ajili ya kuweka dawa na kunyonya vitu walivyotaka. Niliwekewa mipira miwili mdomoni; mmoja katika mapafu na mwingine tumboni; mmoja katika mishipa ya damu ya shingo; na kwa kufanya upasuaji, walichomeka mpira mwingine kifuani hadi katika mshipa wenye kubeba damu isiyokuwa na hewa ya oksijeni kuipeleka kwenye damu (vena cava); mwingine kwenye kalio kwa ajili ya kusafisha damu.
Niliwekewa pia mfuko kwa ajili ya kujisaidia haja kubwa na mfuko maalum kwa ajili ya haja ndogo. Pia niliwekewa sehemu tatu za sindano kwa ajili ya kuingiza dawa na maji maalum yaliyochanganywa na chumvi. Vitu vyote hivyo nilivyofungwa vilinifanya niwe na taswira ya ajabu (utanielewa vyema ukiiona picha inayoambatana na simulizi hii).
Hali iliendelea kuwa ya hatari na ambayo haikubadilika kwa siku nzima. Ilipofika jioni, madaktari walionesha hali ya wasiwasi. Hawakuweza tena kuwatizama moja kwa moja machoni mke wangu au Bis. Hiyo ilikuwa ishara kwamba mambo yalikuwa yanaharibika.
Mwambata wa Kijeshi na mke wake walikuja kutoka London. Hivyo, usiku kulikuwa na watu wanne waliokuwa karibu yangu wakiifuatilia hali yangu. Mke wangu alikuwa amekata tamaa, alikuwa analia kwa nguvu. Kuna nyakati ambapo hata Bis alidondokwa machozi. Kunako saa kumi za usiku, madaktari walimwita Bis kando na kumwambia hali ya baba yake ilikuwa haina njia nyingine ya kuiokoa.
Walitaka kusikia maoni yake kwa vile kuendelea na matibabu kulikuwa ni mateso. Hivyo Bis alikabiliwa na uamuzi mgumu. Kwa kukubaliana na maneno hayo ya madaktari, ingekuwa sawa na kuidhinisha kifo cha baba yake; isitoshe, Bis aliyekuwa msaidizi wa shemasi katika kanisa lake, aliamini kabisa kwamba maamuzi kama haya yalibidi kuachiwa Mungu tu.
Hivyo, aliwasihi madaktari waendelee kufanya juhudi zote. Hali yangu iliendelea kuzorota, hivyo ilipofika saa tano asubuhi, mke wa Mwambata wa Kijeshi alilazimika kumpeleka mke wangu nyumbani ili asifikie mahali akazimia kwa kihoro.
Walipofika huko, waligundua kwamba mkamwana wangu (mke wa mwanangu Bis) alikuwa tayari amewapeleka watoto wake kwa jamaa zake kwa ajili ya matayarisho ya mazishi. Hakutaka kuwajumuisha katika masuala makubwa kama haya.
Kwa kushirikiana, mkamwana na mke wa Mwambata wa Kijeshi walimuogesha mke wangu, wakamlazimisha kula chakula na kumlaza kitandani. Walichokuwa wanakisubiri ni kutoka kwa Bis na DA kuja nyumbani na kuwaambia kwamba nilikuwa nimefariki kwani hadi wakati huo kulikuwa hakuna miujiza iliyokuwa inategemewa.
Usiku wa manane madaktari walimjulisha Bis kwamba mapigo ya moyo na upumuaji wangu vilikuwa vimeteremka sana kiasi kwamba mapigo yalikuwa hayaonekani katika mashine. Hii ilikuwa ni ishara ya wazi kwamba kitabibu nilikuwa nimekufa.
Mtu anapofika katika ukingo wa mambo mbalimbali, ndipo Mungu hutokea. Katika hali halisi, madaktari walikuwa wanaomba ruhusa ya kuachana nami. Huu ndiyo wakati nilipofariki kikweli. Bis alikuwa anabubujikwa machozi. DA alikuwa anafanya kila juhudi kumliwaza akimwambia kwamba nilikuwa sijafa na kwamba nikifa angebeba jukumu la kuurudisha mwili Tanzania kwa mazishi.
Usikose kusoma hapa hapa TanzaniaLeo.com Jumamosi ijayo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment