Waliofanikiwa Hawana Undugu na Mungu, Kwa Nini Wewe Ubweteke?

Mpenzi msomaji wangu, ni ukweli ulio wazi kwamba wengi unaowaona wana maisha mazuri walichagua kuishi hivyo! Waliuchukia umaskini kiasi cha kulazimika kupambana usiku na mchana kuhakikisha wanaondokana na maisha duni.

Hiyo inadhihirisha kwamba kila mtu kama atachagua mafanikio na kuchukia maisha ya utegemezi, anayo nafasi ya kubadili maisha yake na kuondokana na maisha ya utegemezi, maisha ya kimaskini yasiyo na nyuma wala mbele.
Kwa wale wanaoyajua vizuri maandiko matakatifu wanafahamu kwamba, miongoni mwa mambo yanayomchukiza Mungu ni pamoja na kitendo cha mtu ambaye ana uwezo wa kutafuta na akapata kwa kufanya kazi lakini akabweteka na kutegemea msaada.
Wanaozungumziwa hapa ni wale ambao wapowapo tu, hawana kazi za kufanya, hawajishughulishi bali wanategemea kusaidiwa na ndugu zao ambao wamefanikiwa.

Sikatai, kila aliyefanikiwa ana nafasi ya kusaidia ndugu zake pale inapobidi lakini si vibaya kwanza wewe unayehitaji msaada ukajiuliza, umeyapigania vipi maisha yako na ukakwama wapi?
Usikae tu ukabweteka na kutegemea fulani atakusaidia, fahamu na huyo fulani ana majukumu yake. Si kwamba kwa sababu ana uwezo basi kila siku atakuwa akiangalia nani ana tatizo amsaidie, kuna kipindi atakuwa hana uwezo wa kukusaidia, je utaishije?

Waliobahatika kuwa katika nafasi nzuri kimaisha ni mashahidi wa usumbufu wanaoupata kutoka kwa watu wa karibu yao ambao hawataki kujituma. Wao wanategemea tu kusaidiwa licha ya kwamba wakiamua kujituma wanaweza kuondokana na hali duni waliyonayo.

Utamsikia mtu akisema eti maisha ni magumu sana! Jamani, hivi nani kasema maisha ni magumu? Kama ulikuwa hujui elewa ugumu wa maisha tunautengeneza sisi wenyewe na kama tukitaka maisha yawe laini inawezekana!
Kwani hao ambao maisha yao ni mazuri wana tofauti gani na wewe? Unataka kusema wao wana undugu na Mungu hivyo wanapendelewa? Usifikie hatua ya kufikiria hivyo! Wote tuko sawa na kila anayejitahidi anapata baraka za Mungu wala hakuna suala la kupendelewa.

Anza leo kuuchukia utegemezi, anza leo kuchukia maisha ya kuombaomba. Nakuhakikishia kwa kuingiza mawazo hayo kwenye akili yako utaanza kupambana na mwishowe utakuwa ni mtu unayejitegemea.
Yupo kijana mmoja ambaye wakati akisoma alikuwa kila siku anamuomba baba yake pesa ya kuendea shule. Siku moja akakaa na kujiuliza ni lini ataacha kumuomba baba yake pesa?


Kijana huyo alijiuliza swali hilo bila kujua kuwa, baba yake ana wajibu wa kumsaidia mpaka pale atakapokuwa amejimudu. Basi kijana huyo ikawa kila akirudi shule jioni anakwenda kumsaidia baba yake kuuza duka.
Kuanzia hapo akaanza kujiona mwenye amani. Unajua kwa nini? Ni kwa sababu aliona sasa anayo haki ya kupewa pesa kwa sababu alikuwa akisaidia katika kupatikana kwake.

sasa wewe leo hii unaridhikaje kusaidiwa kila siku wakati unao uwezo wa kufanya kazi na kujipatia kipato? Chukia utegemezi, ukiwa kila siku ni mtu wa kusaidiwa unajilemaza na huipi akili yako changamoto za kimaisha.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment