Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ametoa saa 48 kuanzia leo kwa Wakuu wa
Idara wa Halmashauri ya Misungwi ambao wana makazi yao Mwanza mjini
kuhamia mara moja kwenye maeneo ya kazi.
Mongela
alitoa agizo hilo jana wilayani Misungwi alipozungumza na watendaji wa
kata na vijiji, madiwani na wakuu wa Idara wa halmashauri kwenye ziara
yake ya kwanza ya kikazi tangu ateuliwe kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa
Mwanza, na kubaini baadhi ya wakuu wa Idara wanaishi jijini Mwanza.
Alimuagiza
Ofisa Usalama wa Taifa wa Wilaya(DSO) ya Misungwi, Stanslaus Mbile
awafanyie uhakiki wa kina wakuu hao wa Idara kuhamishia makazi yao
Misungwi ili wawahudumie wananchi kwa wakati.
“DSO
nenda nyumba hadi nyumba za wakuu hawa wa Idara na uhakikishe kila mtu
kwa kuwahesabu akiwa na familia yake wamehamia kwenye nyumba zao,
nimekuagiza wewe kwa sababu unajua utaratibu wa vikao vyetu, ukishindwa
kulisimamia hilo kikamilifu nitajua pa kukupeleka,” alisema Mongella.
Alisema
haiingii akilini kwa mtumishi wa umma aliyeajiriwa na kuishi kwa
mshahara unaotokana na kodi za wananchi akiishi nje ya eneo la kazi,
jambo ambalo alisema litaleta shaka katika kuwahudumia wananchi.
“Siwezi
mimi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, halafu naishi Shinyanga, huwezi kuwa
DC wa Misungwi halafu unaishi Sengerema na kwa mtindo huu huwezi
kuwahudumia wananchi,” alisema Mongella na kuongeza:
“Kuanzia
leo (jana) na Wakuu wa Idara wanaokaa nje ya Misungwi watumie siku ya
Karume (jana) kuhamia Misungwi na niwaambie kuwa utaratibu wa Serikali
ya Awamu ya Tano kila mtu awajibike kwenye kipande chake.”
Alisema
hakuhamishiwa mkoani Mwanza kwa lengo la kuhubiri kifo au siku ya
kustaafu kwa watumishi wa umma bali ameteuliwa na Rais John Magufuli
kwenda mkoani Mwanza kufanya kazi za maendeleo ya wananchi na
kushughulika na matatizo ya wananchi na kuyatafutia majawabu.
Aidha,
alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi, Nathaniel
Mshana kuhakikisha watendaji wa kata na vijiji wanaishi kwenye maeneo
yao ya kazi ili iwe rahisi kwa wao kuwahudumia wananchi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment