Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka jana alikuwa mkali
 bungeni akisema yeye si mwizi na kuwabeza wanaomuita hivyo kuwa 
wataisoma namba. 
Profesa Tibaijuka alifikia hatua hiyo baada ya 
kuhamaki kutokana na baadhi ya wabunge wa upinzani kupaza sauti na 
kumuita mwizi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na 
Sheria. 
Profesa Tibaijuka alianza kwa kuwataka wabunge wamuunge 
mkono Rais John Magufuli kwa kuwa amechaguliwa na wananchi.
“Wenzetu 
ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi (upinzani) wana haki ya kusema 
wanayoyasema, lakini hata sisi tuna haki ya kuyaweka vizuri ili 
yaeleweke kwa wananchi,” alisema. 
Profesa Tibaijuka alisema 
upinzani ukifilisika utabaki kukemea kwa sababu ni lazima tu useme kitu,
 Bunge linageuka kijiwe na bungeni si mahali pa kupeleka hoja za 
vijiweni. 
Kauli hiyo iliwakera wabunge wa upinzani ambao walianza kupaza sauti zao dhidi yake, hali iliyoonekana kumchanganya. 
Akirejea
 hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu kuwa 
Tanganyika inainyonya Zanzibar na kuifanya koloni lake, Profesa 
Tibaijuka alihoji: “Tanganyika inainyonya Zanzibar katika lipi? Hili ni 
jambo la kujiuliza. Nimejiuliza mimi kama mchumi. Kazi yangu ya kwanza 
nyinyi mnanijua nilikuwa kwenye shirika la makazi duniani, hamjui kwamba
 nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia?” alihoji. 
Kutokana
 na zomeazomea kuendelea, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliingilia kati: 
“Waheshimiwa wabunge namlinda mzungumzaji, naomba muwe wavumilivu. 
Mheshimiwa Profesa endelea."
“Kwa wale wanaosema nimeiba mtaisoma namba, mimi si mtu wa kutishwa na vitu vya ovyoovyo. 
"Mimi
 sitishwi na hoja za ovyoovyo, huyo (mtu) akaisome namba. Nasimama hapa 
kwa sababu nataka nitetee vitu. Mtu anapopotosha anaweza kuleta hatari. 
Tanganyika kwa mtizamo wa kiuchumi haiwezi kuinyonya Zanzibar. 
“Katika
 Dunia ya ustaarabu unasikia hoja. Lissu hapa angeweza kuzomewa, lakini 
wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa,” alisema huku baadhi ya 
wabunge wakiendelea kumzomea. 
Tibaijuka aliwahi kuwa waziri wa 
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa utawala wa Rais Jakaya 
Kikwete na aliondolewa baada ya kutuhumiwa kupata mgawo wa fedha za 
Tegeta Escrow. 
 TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]

0 comments:
Post a Comment