Mshambuliaji wa Taifa Stars Mbwana Samatta
Khadija Mngwai, Dar es SalaamKUFUATIA mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kufanikiwa kuifungia timu yake ya Genk ya Ubelgiji mabao mawili hadi sasa, imebidi apewe zigo la kuifunga Chad katika mchezo wa keshokutwa Jumatano ugenini.
Stars inatarajia kuvaana na Chad ugenini katika mchezo wa kuwania kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ambapo wachezaji wataondoka kwa mafungu huku kundi lingine likitarajiwa kuondoka nchini leo Jumatatu na Samatta akitarajiwa kujiunga na timu juu kwa juu.
Aidha, Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe wanatarajiwa kuwa tegemeo katika kusaka mabao ya Stars.
Kocha wa JKT Ruvu, Abdalah Kibadeni ambaye ni Mshauri Mkuu wa Benchi la Ufundi la Stars, amefunguka kuwa ana imani kubwa na Stars kufanya vizuri katika mchezo wake na Chad kutokana na uwepo wa Ulimwengu na Samatta ambaye ameonekana kufanya vyema katika klabu yake mpya ya Genk.
“Mchezo utakuwa mgumu lakini nina imani timu yetu itafanya vyema katika mchezo huo kufuatia uwepo wa Samatta na Ulimwengu katika timu yetu hiyo.
“Vilevile kuna wachezaji wengine wazuri ambao kocha (Charles Boniface Mkwasa) amewachagua kutoka Yanga, Simba na Azam ambao wameonyesha kiwango kizuri msimu huu na watafanya vyema,” alisema Kibadeni.
Wakati huohuo, timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars jana ilitoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Zimbabwe na kuaga michuano ya kufuzu Fainali za Mataifa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mchezo wa awali kupigwa 2-1.
Kikosi cha Twiga klinatarajiwa kutua leo nchini mchana kwa usafiri wa Shirika la Ndege ya Fastjet.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment