Freeman Mbowe na Zitto Kabwe Wamkaba Koo Spika wa Bunge Ndungai

Ni wazi kuwa uamuzi wa upinzani kutoshiriki uchaguzi wa wenyeviti wa kamati mbili wanazopaswa kuziongoza, umeliweka Bunge katika mtego wa kuonekana haliwezi kuisimamia vizuri Serikali.

Kutokana na hali hiyo, kamati hizo za usimamizi (Oversight), ile ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zimeendelea kusimamiwa na makamu wenyeviti ambao wanatoka chama tawala, ikiwa ni siku 81 tangu kufanyika uteuzi wa wajumbe wa kamati 18 za chombo hicho.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alilieleza Mwananchi jana kuwa kanuni na taratibu zinawaruhusu wapinzani kupendekeza majina ya watu wanaotaka kuwa wenyeviti wa kamati hizo, lakini hawapo tayari kupangiwa viongozi na CCM.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), ambaye amekuwa mwenyekiti wa PAC katika Bunge la 10, Zitto Kabwe alisema Bunge halitendi haki kwa kuacha kamati hizo bila uongozi.

Alisema jambo hilo lina madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na masuala mbalimbali nyeti kutowekwa wazi kwa kuwa wapinzani hawapo.

Kwa mujibu wa mabunge ya jumuiya za madola, kamati hizo lazima ziongozwe na wabunge kutoka upinzani, lakini hali imekuwa tofauti katika Bunge la sasa baada upinzani kushinikiza kuchagua viongozi wake badala ya kupangiwa.

Lakini, Spika wa Bunge, Job Ndugai alilieleza gazeti hili kuwa aliteua wabunge kwenye kamati kama walivyoomba na kati yao wapo wanaoweza kuwa wenyeviti na kushangaa vyama vinavyounda Ukawa kupinga suala hilo.

Tangu Februari 21, kamati hizo zimekuwa zikiendelea na shughuli zake kama kawaida huku zikiongozwa na makamu wenyeviti kutoka CCM.

Pamoja na hivi karibuni Ndugai kufanya mabadiliko ya wajumbe wa kamati kadhaa za Bunge kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa wazi, hakubadili wajumbe wa kamati hizo licha ya kuwapo malalamiko dhidi yake.

Katika mkutano uliopita wa Bunge, pia iliibuliwa hoja ya majukumu ya PAC kuhamishiwa katika kamati mpya ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) inayoongozwa na CCM, jambo ambalo lilipingwa na upinzani wakieleza kuwa kanuni za Bunge hazijabadilishwa kuruhusu jambo hilo.

Akizungumzia suala hilo, Mbowe alisema: “Kuna kanuni zinazoeleza utaratibu wa upinzani kupata viongozi katika kamati na Bunge linatambua suala hilo, lakini kinyume chake CCM imekuwa ikiingilia na kutaka kutuchagulia viongozi.”

Mbowe alisema si kweli kuwa wabunge wa upinzani walioteuliwa katika kamati za PAC na LAAC hawana uwezo wa kuwa wenyeviti.

“Lakini lazima tutambue kuwa wabunge wanatofautiana uwezo na pia hatutaki watuchagulie watu. Kamati zetu, iweje tuchaguliwe watu?” alihoji.

Alisema hasara ya kupangiwa viongozi na CCM imewahi kujitokeza miaka ya nyuma baada ya walioziongoza kamati hizo kutumiwa kwa faida ya Serikali.

Alibainisha kuwa wamekutana mara kadhaa na Ndugai kuzungumzia suala hilo, lakini amekuwa akiwaeleza kuwa atalishughulikia.

“Mpaka sasa taarifa za CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) kuhusu mashirika ya umma hazijakaaguliwa. Hivi wanaogopa nini wapinzani kujipangia viongozi wa kamati hizi? Mwakilishi wa upinzani atachaguliwa vipi na CCM,” alisema Mbowe.

Alisema kuwa katika mkutano wa Bunge unaoanza Aprili 19, wataliibua suala hilo na kuendelea kuzungumza na ofisi ya Spika kujua hatima yake na baada ya hapo ndiyo watatoa msimamo wao wa mwisho.

Kwa upande wake, Ndugai alisema: “Kila mbunge alichagua anataka kuwa kamati ipi na mimi niliwapanga kulingana na walivyoomba. Hakuna niliyemteua ambaye alilalamika kuwa na uwezo mdogo katika kamati aliyopo na kutaka ahamishwe.”

Alisema upinzani unaonekana wazi kutowaamini wajumbe wake waliopo katika kamati ya PAC na LAAC na kusisitiza kuwa hana ushauri wowote kwao, kwa kuwa kazi za kamati hizo zinaendelea kama kawaida chini ya makamu wenyeviti.

“Kuna aina ya sifa ambazo hazina tija. Ukiwachambua wajumbe wa upinzani waliopo katika kamati hizi mbili, utabaini kuwa wana uwezo mkubwa sana wa kuwa wenyeviti,” alisema.

Makamu mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema: “Sijui wana malengo gani maana wajumbe wa upinzani waliopo katika kamati yetu wana uwezo mzuri tu sijui kwanini hawataki kuaminiana.”

Alisema kila mbunge anaweza kuwa mwenyekiti wa kamati na kuongeza kuwa hata wabunge maarufu walipewa nafasi katika kamati ndipo wakaonyesha uwezo wao wa uongozi.

Athari iliyopo
Akieleza athari ya CCM kuongoza kamati hizo, Zitto alisema: “Athari yake ni Serikali kujifanyia inavyotaka. Kunapokuwa na jicho la upinzani wananchi watajua kinachoendelea ila kama wapo CCM peke yao mambo mengi yatafichwa.”

Alisema kamati ya PAC ina mamlaka ya kisheria ya kupitisha bajeti ya ofisi ya CAG, lakini kutokana na wapinzani kutokuwapo Serikali imepunguza bajeti ya ofisi hiyo kwa asilimia 60 na hakuna anayeweza kuhoji.

“Bajeti ya Bunge pia imepunguzwa kwa asilimia 50 na mahakama asilimia 50. Jambo hili lina madhara makubwa wananchi hawajui tu na pia nasikitika kuona hata wapinzani nao hawajali,” alisema Zitto.

Alisema kitendo cha ofisi ya CAG kupunguziwa bajeti kinaashiria kwamba Serikali haitaki kutazamwa na kusimamiwa, huku akisisitiza kama wapinzani wangekuwa wanaiongoza kamati hiyo ni wazi kuwa suala hilo lingeibua mjadala mkali.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment