Mkazi wa Toraja, Sulawesi Kusini, nchini Indonesia akiwavisha nguo ndugu zake waliokufa siku za nyuma.
UNAWEZA usiamini! Huko Toraja, Sulawesi Kusini, nchini Indonesia,
wakazi wa huko wana mila ambayo kuna wakati wanawafukua ndugu zao
waliokufa – wakiwemo watoto wadogo – wakawaosha, wakawafanyia kila usafi
na kuwavisha nguo mpya za kuvutia.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo ambao husema wafu hao huendelea
kuishi katika mioyo na akili zao, wanadai marehemu hao huendelea
kutembea maeneo mbalimbali duniani wakiwa kama misukule au mizimu.
Wakati wa utaratibu huo ambao unajulikana kama Ma’nene, maiti hao
hubebwa kutoka sehemu walizofia au kuzikwa na baada ya kufanyiwa
mchakato huo wa kijadi, hutembezwa maeneo mbalimbali ya Jimbo la
Sulawesi wakiwa katika mstari mmoja.
Baada ya utamaduni huo, maiti hao hurejeshwa katika majeneza ambayo
hukarabatiwa ikiwa yameharibika wakati wa kuwatoa maiti au majeneza
mapya hununuliwa kwa ajili ya kuwahifadhi tena.
Utaratibu huo wa Ma’nene ambao humaanisha ‘Sherehe ya Kuwasafisha
Maiti’, hufanywa na watu wa Toraja kwa imani ya kuzirudisha roho za wafu
katika vijiji vyao.
Hivyo, iwapo mtu alifariki akiwa safarini, familia huwajibika kwenda
mahali alikofia na kumsindikiza kurejea nyumbani kwa kumtembeza hadi
kijijini.
Katika siku za nyuma, watu wa eneo hilo walikuwa wanaogopa kusafiri
mbali, wakiogopa kwamba pindi wakifia huko wasingeweza kurejea vijijini
kwao.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment