Haruna Niyonzima
Ibrahim Mussa, Dar es SalaamLICHA ya kufunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, amefunguka kuwa amecheza mchezo huo huku akisumbuliwa na maumivu ya shingo kiasi kwamba alikuwa akigeuka kama roboti.
Niyonzima ambaye alikuwa nje akisumbuliwa na malaria, hivi karibuni, alifunga bao hilo la ushindi lakini alikiri kuwa alikuwa na wakati mgumu uwanjani japokuwa wengi hawakujua hilo.
Kitendo cha Niyonzima kucheza akiwa na maumivu hayo huku akigeuka kama roboti, kingeweza kumpa maumivu zaidi kama asingekuwa makini kwa kuwa mchezo wa soka unatumia nguvu kucheza.
Kukosekana kwa Niyonzima katika mchezo dhidi ya Al Ahly, wiki iliyopita kuliwafanya mashabiki wengi wa timu hiyo kuamini kuwa pengo lake lilikuwa kubwa na kuchangia matokeo ya sare ya bao 1-1.
“Ushindi ndiyo kitu cha muhimu ambacho tulikuwa tunakipigania, nimecheza nikiwa na maumivu ya shingo kiasi cha kunifanya nishindwe kugeuka vizuri mara kwa mara na kuweza kupambana vizuri.
“Nahisi siyo tatizo la kutisha sana mpaka linifanye nishindwe kucheza mchezo wowote ingawa bado maumivu nayasikia mpaka sasa, nimekuwa nikigeuka mwili mzima.
“Maumivu haya yalianza leo hii asubuhi (juzi), nilipouliza kwa daktari niliambiwa yawezekana niliilalia vibaya shingo,” alisema Niyonzima ambaye hata hivyo aliendelea kulalamika kuwa bado anasikia maumivu na hawezi kugeuka vizuri kwa haraka.
Alipoulizwa Daktari wa Yanga, Edward Bavo alisema: “Ni kweli alikuwa anaumwa lakini mpaka muda wa kwenda uwanjani alikuwa fiti, yawezekana ni maumivu ya kawaida ila tutamfanyia uchunguzi zaidi kujua tatizo zaidi.”
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment