Makonda alisema hayo jana wakati wa kuaga mwili wa Kabwe kwenye ukumbi wa Karimjee, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Mamba Mpinji wilayani Same, Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayofanyika leo.
Awali, mmoja kati ya wanafamilia alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa familia haihitaji ushiriki wowote wa Serikali kwenye maandalizi ya mazishi hayo.
Alitoa kauli hiyo kutokana na Kabwe kusimamishwa kazi kwa amri ya Rais John Magufuli baada ya kusomewa makosa yake na Makonda mbele ya umati wa watu wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni.
Hata hivyo, ndugu wengine walikanusha kauli hiyo na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na familia katika kumuuguza Kabwe na kwamba kifo chake hakikutokana na kusimamishwa kazi kwa kuwa wakati uamuzi huo unatangazwa alishaanza kuugua.
Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Makonda aliipongeza familia ya marehemu, akisema imevuka mtihani ambao Watanzania wengi wangeshindwa kutokana na kulivisha tukio hilo sura ya tofauti wakati wa msiba.
“Baadhi ya watu waliniambia nisihudhurie msiba na hata baadhi ya vyombo vya habari vikatengeneza mazingira vinayoyaona kwamba yanafaa,” alisema Makonda.
“Ila nitaendelea kutimiza wajibu wangu na wanafamilia mmeliona hilo na niwape pongezi.”
Makonda aliwasihi Watanzania kuwa watulivu na kushauri watumishi wa umma kuwa waadilifu katika kazi zao.
“Maadam Kabwe amelala, tusitumie fursa hii kumrundikia mizigo eti tukifikiri kwamba tutakuwa salama mbele za Mungu. Tuhakikishe kila mmoja anafanya kwa nafasi yake na kwa wajibu wake ili tusiwatwishe mizigo watu waliotangulia mbele za haki.”
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za kidini, wafanyakazi wa umma na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Akitoa salamu za Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema kifo cha Kabwe kimewasikitisha na kwamba ameacha pengo, si kwa familia pekee bali hata serikalini.
Simbachawene alisema Kabwe amekuwa mtumishi wa umma kwa miaka 37 na kwamba yapo mengi aliyoyafanya, mazuri na mabaya lakini kwa sasa yakumbukwe yale mema na kuyaendeleza.
“Rais (Magufuli) na Serikali tunatambua mchango mkubwa alioutoa marehemu (Kabwe) katika utumishi wake kwa miaka 37, tunaahidi kuyaendeleza yale yote aliyoyaacha,” alisema Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Kibakwe (CCM) mkoani Dodoma
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment