Rufani ya Jamhuri Dhidi ya Bosi wa Zamani wa TRA na Wenzake Kusikilzwa Jumanne ya Wiki Ijayo

Mahakama ya Rufani imepanga kusikiliza rufaa dhidi ya Mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake, Shose Sinare na Sioi Solomon juma lijalo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mahakama ya Rufani, rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Jumanne Mei 31 na chini ya majaji watatu Bernard Luanda, Salum Masatti na Semistocles Kaijage.

Rufaa hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyotupa rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao shtaka la kutakatisha fedha.

Kitilya na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kutakatisha Dola za Marekani 6 milioni.

Hata hivyo, baadaye Mahakama ya Kisutu iliwafutia shtaka la kutakatisha fedha, baada ya mawakili wa washtakiwa hao kupinga uhalali wa shtaka hilo, uamuzi huo ulipingwa na DPP na kukata rufaa Mahakama Kuu akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, lakini mawakili wa washtakiwa hao waliweka pingamizi wakidai kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu hauwezi kukatiwa rufaa kwa kuwa ni uamuzi mdogo ambao haumalizi kesi.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Moses Mzuna, ilikubaliana na pingamizi la mawakili wa washtakiwa hao na ikaitupa rufaa hiyo na kuelekeza DPP arudi Mahakama Kisutu aombe kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka ili kurekebisha shtaka la kutatakisha fedha lililofutwa.

DPP hakuridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama Kuu ndipo akaamua kusonga mbele na kukata rufaa nyingine Mahakama ya Rufani.

Kitilya na wenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Katika hatua nyingine, Mahakama ya Rufani imefufua kesi ya uchaguzi dhidi ya Mbunge wa Mbarali mkoani Mbeya, Haroun Mullah iliyokuwa imetupwa na Mahakama Kuu na kuamuru isikilizwe upya.

Mahakama ya Rufani imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya katika uamuzi wake wa rufaa iliyofunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika kinyang’anyiro Uchaguzi Mkuu 2015, Liberatus Laurent Mwang’ombe.

Mwang’ombe alikata rufaa hiyo baada ya kesi yake ya msingi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mullah kutupwa na Mahakama Kuu, kutokana na kutokuwasilisha baadhi ya vielelezo vya ushahidi wa kesi yake.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Atuganile Ngwale, ilisema kutokana na kutokuwapo vielelezo hivyo ambavyo ni fomu ya matokeo na kadi ya gari la mdaiwa (Mbunge Mullah) kunaifanya kesi hiyo kukosa msingi wa sababu za madai.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa Mahakama Kuu ilikosea kuitupa kesi hiyo, kwani ilikuwa bado katika hatua za awali na ilikuwa haijaanza kusikilizwa, hivyo mdai alikuwa na nafasi ya kuwasilisha vielelezo hivyo.

Hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa juzi na majaji watatu Engela Kileo, Katherine Oriyo na Semistocles Kaijage, iliamua kesi hiyo isikilizwe upya.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment