Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza bajeti ya Serikali hiyo ya Sh
bilioni 841.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017; na kupandisha mshahara kwa
kima cha chini kutoka Sh 150,000 hadi Sh 300,000.
Hatua
hiyo imelenga kuongeza ufanisi na kupambana na ugumu wa maisha kwa
wafanyakazi wake, kubana matumizi ya ndani na kuifanya nchi kuwa ya
viwanda.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Khalid Salum Mohamed ndiye aliwasilisha bajeti hiyo katika Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.
Alisema vipaumbele katika bajeti hiyo ni katika kuimarisha sekta ya elimu, afya na miundombinu ya bandari na uwanja wa ndege.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakadiria kutumia Sh bilioni 841.5
kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 445.6 kwa
kazi za kawaida na Sh bilioni 395.9 kwa kazi za maendeleo.
Alisema
katika mwaka wa fedha 2016-2017 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo
katika mchakato wa kukamilisha na kuanza kwa miradi miwili mikubwa ya
miundombinu, ambayo ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan
Karume katika jengo la abiria.
Aidha
alisema ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mpigaduri, utasaidia kuongeza
mapato na ajira kwa wananchi wa Zanzibar mara utakapomalizika.
Dk
Salum alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 inakabiliwa na
changamoto mbalimbali, ikiwamo kupungua kwa fedha kutoka kwa washiriki
wa maendeleo; na ndiyo maana bajeti hiyo itajikita zaidi katika kuweka
kipaumbele cha makusanyo ya kodi ya ndani.
“Tumeweka
kipaumbele zaidi katika makusanyo ya kodi kupitia vyanzo vyake, ambapo
taasisi za ukusanyaji kodi Mamlaka ya Mapato (TRA) na Bodi ya Mapato
Zanzibar (ZRB) tumezipa majukumu makubwa zaidi katika makusanyo ya
kodi,” alisema Dk Salum.
Alifahamisha
kwamba TRA inatarajiwa kukusanya Sh bilioni 188.8, wakati ZRB
itakusanya Sh bilioni 237.4. Waziri huyo alisema muelekeo wa uchumi wa
Zanzibar ni kufikia uchumi wa kati na usipungue asilimia nane kwa mwaka
na kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Alisema SMZ imelenga Zanzibar kuwa nchi ya viwanda katika sekta ya kilimo na uvuvi na kuimarisha sekta ya utalii.
Aidha,
alisema serikali imesikia kilio cha kupungiza kodi ya mishahara ya
wafanyakazi zaidi kipato cha chini, ambapo sasa kitapunguzwa kutoka
asilimia 13 hadi 9.
Salum
alitangaza kwamba katika bajeti ya fedha kwa mwaka 2016-2017,
hakutakuwa na ongezeko la kodi kwa lengo la kupunguza mzigo kwa
wananchi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment