TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezitumia
salamu za pole familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 12 waliopoteza
maisha kufuatia ajali mbili zilizotokea katika eneo moja la VETA Dakawa,
Tarafa ya Dumila, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Ajali
ya kwanza imetokea majira ya saa 11:30 jioni ya tarehe 30 Juni, 2016
ambapo watu 5 wamefariki dunia kufuatia malori mawili, mojawapo likiwa
na shehena ya mafuta kugongana na kisha kuwaka moto, na ajali ya pili
ikatokea hapohapo majira ya saa 10:00 alfajiri ya tarehe 01 Julai, 2016
baada ya basi la kampuni ya Otta High Class kuligonga lori la mafuta
lililokuwa likiungua moto na kusababisha vifo vya watu 7 mpaka sasa.
Katika
salamu zake kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe,
Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko taarifa za
vifo vya watu hao ambao licha ya taifa kupoteza nguvu kazi muhimu,
ndugu, jamaa na marafiki wamepoteza watu waliowategemea na wapendwa wao.
“Ndugu
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Steven Kebwe naomba unifikishie salamu
zangu za pole kwa wote waliopatwa na msiba na uwaambie naunga nao katika
kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Pia nawaombea wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu na Mwenyezi awapumzishe marehemu wote mahali pema peponi, Amina” amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amewaombea majeruhi wote waliolazwa hospitali na wale
wanaoendelea kupata matibabu wakiwa majumbani, kupona haraka ili
waendelee na kazi zao za kila siku.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
02 Julai, 2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment