MAHAKAMA Maalumu ya kushughulikia Makosa ya Rushwa na Ufisadi, inaanza rasmi leo Julai mosi.
Pamoja
na kuanza kwa mahakama hiyo, serikali imeanza mchakato kuifanyia
marekebisho Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ya
Mwaka 2007 ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa sasa.
Mahakama
hiyo iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 na imo katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha
Mapinduzi, itaimarisha zaidi taasisi za uwajibikaji zinazohusika na
mapambano dhidi ya rushwa.
Ahadi
hiyo ambayo inatimizwa ndani ya kipindi cha miezi isiyozidi saba tangu
Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni sehemu ya mapambano ya
kujenga misingi ya uchumi kwa kudhibiti rushwa na mianya yake na kuleta
uwajibikaji.
Akiahirisha Bunge jana mjini Dodoma,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema utekelezaji wa ahadi hiyo
unakwenda sambamba na kuonesha dhamira ya serikali ya kushughulikia
makosa ya rushwa na kuweka misingi imara ya uwajibikaji katika sekta
zote.
“Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kufanya uhalifu huo yaani kuwa deterrent,”
alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa kuwapo kwake kutahamasisha
wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila shaka huku umuhimu kwao, ikiwa
ni kulipa kodi.
Akielezea
umuhimu wa mahakama hiyo, alisema kwamba itasaidia kuendeleza nia ya
serikali ya watu kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Akielezea
umuhimu wa kodi, alisema kuna mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji
wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za serikali na hivyo
serikali itaendelea ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya
ukwepaji kodi.
Aidha,
alisema serikali itaanzisha Kikosi Maalumu cha kufuatilia kwa karibu
matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) za kutoa risiti kila
mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma na kuhakikisha kuwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA)
wanashirikiana na Wakala wa Serikali wa Serikali Mtandao kutekeleza
mfumo wa kuwa na dirisha moja na pia kudhibiti kikamilifu mizigo
inayoingia na kutoka bandari kavu.
Udhibiti wa matumizi
Akizungumzia
matumizi, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea na kudhibiti matumizi
yasiyokuwa ya lazima na kufuatilia bajeti na matumizi ya fedha za umma.
Na
ili kufanikisha hilo, itafanya mapitio ya majukumu ya wizara na taasisi
za umma ili kuwianisha majukumu ya vyombo vya serikali na hivyo
kupunguza gharama za uendeshaji.
Aidha,
uhakiki wa wafanyakazi utaendelea na watendaji wakitakiwa wanadhibiti
matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya fungu husika
lililoidhinishwa na Bunge.
Aidha,
Waziri Mkuu aliagiza halmashauri zote nchini kuanzia leo kuhakikisha
kwamba zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato,
kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha
makusanyo iwe yanafanywa na halmashauri au kupitia wakala wake.
Waziri
Mkuu alisema wabunge wamepitisha Bajeti ya Serikali inayotegemea sana
ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje na
kuhimiza uwajibikaji katika kuongeza juhudi za kukusanya na kupanua wigo
wa kutoza kodi ili mapato yaongezeke.
Aidha,
alisema ipo haja ya wananchi kudai risiti kwa huduma mbalimbali
wanazonunua na kushirikiana na serikali kubaini wakwepa kodi na kuziba
mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.
Aliwataka
watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa maadili katika maeneo yao
wakijenga utamaduni wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika
utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija.
Mpango wa Maendeleo
Akizungumzia
maeneo manne ya Mpango wa Maendeleo, Waziri Mkuu alisema kwa sasa
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka msingi kupitia Mpango wa Pili wa
Maendeleo ya Taifa wa kukuza na kujenga uchumi wa viwanda kwa kuweka
mazingira yatakayochochea maendeleo ya viwanda.
Aidha,
imejiweka katika hali ya kufungamanisha maendeleo ya uchumi na
maendeleo ya watu kwa kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ni bora na
inayojenga msingi wa rasilimali watu wanaohitajika kuipeleka nchi katika
uchumi wa kati.
Alisema
ili kufanikisha hayo serikali itaimarisha mifumo ya kisheria kuwa
rafiki na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje huku ikiimarisha
miundombinu ili iweze kutumika kirahisi na kupunguza gharama zake.
Ili
kufanikisha ufanisi na tija, Waziri Mkuu alisema serikali itaimarisha
usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya mpango wenyewe wa maendeleo mara
kwa mara.
Ili
kufanikiwa ametaka tabia ya vijana kushinda katika pombe na kucheza
pool table kuachwa na kuwataka viongozi waliochaguliwa sasa wilayani na
mikoani kuhakikisha kwamba maeneo ya starehe hayafunguliwi wakati wa
muda wa kazi ili vijana washiriki katika uzalishaji mali.
Akizungumzia
mkakati wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, Waziri Mkuu alisema serikali
itategemea zaidi sekta binafsi kama injini ya ukuzaji uchumi na
maendeleo na kwamba serikali haitajiingiza moja kwa moja katika kujenga
viwanda na kufanya biashara.
Miradi ya umeme
Akizungumzia
uimarishaji wa uchumi kwa kuwa na uhakika wa nichati hadi vijijini,
alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuyapatia maeneo yaliyo nje
ya gridi ya taifa nishati bora ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwani.
Alisema
Serikali ya Uingereza na Sweden zinachangia katika kuhakikisha kwamba
mifumo hiyo ya kupeleka umeme maeneo yaliyo nje ya gridi inafanikiwa.
Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh trilioni moja kutoka ndani na
benki ya dunia kwa ajili ya kuendeleza nishati vijijini.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment