Hali si shwari kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) baada
ya wafanyabiashara wa mataifa yanayotumia Bandari ya Dar es Salaam
kutafuta sehemu nyingine kiasi cha kusababisha kiwango cha mizigo
kupungua kwa asilimia 50.
Bandari hiyo, ambayo ni maarufu kwa
usafirishaji wa mizigo inayokwenda na kutoka nchi za Malawi, Congo,
Uganda, Burundi na Rwanda, imekumbwa na kadhia hiyo baada ya
wafanyabiashara wa nchi hizo kuamua kutumia bandari nyingine za Beira,
Msumbiji na Durban ya Afrika Kusini.
Kaimu Meneja wa Bandari ya
Dar es Salaam, Hebel Mhanga alisema hali ya biashara kwa sasa si nzuri
kwa kuwa mtiririko wa shehena za mizigo umepungua ikilinganishwa na
miaka iliyopita.
“Miaka yote shehena ya mizigo bandarini ilikuwa
ikiongezeka kwa kati ya asilimia 10 mpaka 11, lakini sasa imeshuka
mpaka kufikia asilimia 50,” alisema Mhanga kwenye semnina ya wahariri
iliyofanyika ofisi za bandari hiyo jana.
Mhanga alitoa mfano wa
shehena iliyokuwa ikisafirishwa na wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC), kuwa imepungua kwa asilimia 50 huku mizigo
ya wafanyabiashara wa Zambia ikipungua kwa asilimia 46.
Alitaja
sababu zilizochangia kuporomoka kwa biashara hiyo kuwa ni pamoja na
wafanyabiashara hao kuanza kukatwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Alisema
tangu sheria ya ulipaji wa VAT ilipopitishwa mwaka jana, wasafirishaji
wote wanaotumia bandari hata wale ambao mizigo yao inasafirishwa kwenda
nchi jirani, wanalazimika kulipia kodi hiyo.
Sababu nyingine ni
utaratibu wa himaya moja ya forodha kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Alisema baada ya kuona mfumo huo unafaa, Tanzania
iliamua kuutumia kwa nchi nyingine ambazo hazipo katika jumuiya hiyo.
Alisema
katika utaratibu huo, nchi zote zinakuwa na mwakilishi katika ofisi za
TPA na masuala ya kodi na mizigo yote inalipiwa ushuru nchini kabla ya
kusafirishwa kwenda nchi zao.
“Hili limekuwa mwiba kwa wenzetu
wa DRC, kwani nchini mwao mfumo wa ukusanyaji kodi unatoa mianya ya
ukwepaji, kwa hiyo kwa kutumia njia hii ni wazi kuwa kila mzigo
utalipiwa hapa nchini kabla haujasafirishwa, jambo wanaloona
linalowaongezea gharama za uendeshaji,” alisema.
Mhanga alisema
kutokana na hali hiyo, kwa sasa wafanyabiashara hao wameamua kutumia
bandari za nchi nyingine kupitisha mizigo yao, akizitaja kuwa ni Durban
na Beira.
Sababu nyingine aliyoitaja ni kushuka kwa thamani ya
Randi dhidi ya Dola ya Marekani, kitu alichosema kinawafanya
wasafirishaji kuona kwamba wakipitishia mizigo yao Dar es Salaam
wanatumia fedha nyingi kuliko Durban.
“Ulipaji wetu
unawalazimisha wafanyabiashara watumie Dola wakati wao wanatumia Randi
ya Afrika Kusini na sasa imeshuka, hivyo njia rahisi kwao ni kutumia
Bandari ya Durban kwa kuwa watapunguza gharama za usafirishaji,”
alisema.
Alisema sababu ya nne ni kukamilika kwa ujenzi wa njia ya reli kutoka Malawi hadi Beira.
Alisema
usafirishaji mizigo kwa njia ya reli ni nafuu kwa kuwa unapunguza
gharama kwa asilimia 30 na pia hutumia siku chache hivyo wafanyabiashara
wengi sasa wanatumia bandari ya Beira badala ya Dar es Salaam.
“Kutofanya vizuri kwa reli yetu ni kikwazo kikubwa kwa biashara ya
bandari. Mfano hadi Desemba 2015, jumla ya tani 14.8 zilipita bandari
yetu, lakini ni asilimia 0.01 pekee ndiyo iliyosafirishwa kwa njia ya
reli na asilimia 99.9 ilisafirishwa kwa barabara,” alisema meneja huyo.
Meneja huyo alisema ili kunusuru hali hiyo, busara inahitajika zaidi, ikiwa ni pamoja na kupitia upya sheria hiyo ya VAT.
Alisema
kwa upande wao wameshafanya maboresho ili kuvutia wawekezaji kuja
nchini, ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia tofauti na
awali.
Alisema kwa sasa wamezindua mfumo mpya unaojulikana kama
‘Habour View’ unaosaidia kupokea taarifa zote za meli, mizigo na ulipaji
hivyo mteja anaweza kulipia kwa njia za benki na simu.
Alisema wamefupisha muda wa kushusha mzigo katika meli hadi kufika siku mbili tofauti na awali ilipokuwa inachukua siku sita.
Alisema
kwa upande wa shehena ya magari, mwaka 2010 uwezo ulikuwa ni kushusha
magari 200 lakini kwa sasa wana uwezo wa kushusha magari 700.
Awali, Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Fransisca Muhindi alishauri Serikali kuwekeza katika kutangaza bandari hiyo ili kuinusuru.
“Wenzetu hawalali, wanafanya biashara ya ‘door to door market’(nyumba
kwa nyumba), wanawekeza kiasi kikubwa. Ni bahati mbaya sana sisi
hatuwekezi. Kuna usemi unasema wekeza shilingi ili upate shilingi,”
alisema.
Alisema kwa sasa mzigo wa shaba ambao awali ulikuwa
asilimia 60 ya mizigo yote bandarini umeshuka hadi kufikia asilimia 15
huku sababu kubwa ikiwa ni reli.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment