Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za pongezi Rais Mteule wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein,
kufuatia ushindi alioupata katika marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Rais wa
Zanzibar, uliofanyika jana tarehe 20 Machi, 2016.
Katika
salamu hizo Rais Magufuli amesema ushindi wa Dkt. Shein umedhihirisha
imani na matumaini makubwa waliyonayo wazanzibari kwake na kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Aidha,
Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki katika
uchaguzi huo kwa amani na utulivu, na hatimaye kumpata mshindi wa kiti
cha Urais ambaye atawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
"Naomba
nikupongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais Mteule Dkt. Ali Mohamed Shein kwa
ushindi ulioupata, ushindi ambao umeonesha kuwa wananchi wa Zanzibar
bado wanahitaji uwaongoze kwa kipindi kingine cha miaka mitano" Amesema Rais Magufuli.
Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli pia ameahidi kuwa serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na amewataka Wazanzibari wote kujielekeza
katika maendeleo kwa kuwa uchaguzi umekwisha.
"Ndugu
zangu wa Zanzibar uchaguzi umekwisha, kilichobaki sasa ni kushirikiana
na serikali yenu kuijenga Zanzibar na ninaamini mnao wakati mzuri wa
kuijenga Zanzibar yenye maendeleo chini ya uongozi wa Dkt. Ali Mohamed
Shein" amesisitiza Dkt. Magufuli
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment