Serikali
imesema vigogo wa juu katika utumishi wa umma, watakaobainika kuhusika
kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa,
watafunguliwa kesi ya jinai.
Aidha,
imesema ifikapo Julai mosi, mwaka huu Halmashauri zote nchini ziwe
zimefunga na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato
yake ya ndani na zimetakiwa kusitisha ukusanyaji kwa njia ya mawakala.
Katika
hatua nyingine imesema hadi kufikia Machi, 2016, watumishi 90
wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine kufikishwa
mahakamani kwa kukiuka taratibu na sheria za kazi wakiwemo wakurugenzi
watendaji (DED) wa halmashauri watano ambao wamevuliwa madaraka.
Hayo
yalisemwa kwa wakati tofauti na mawaziri wawili katika Ofisi ya Rais,
walipowasilisha hotuba za bajeti kwa ofisi zao kwa mwaka ujao wa fedha
bungeni mjini Dodoma jana.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki
akiwasilisha hotuba ya ofisi hiyo, alisema kuanzia sasa kiongozi wa
serikali wakiwemo wa ngazi za juu watakaobainika kuhusika kwa njia moja
au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa watafunguliwa
kesi za jinai.
Waziri
huyo alisema uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote unahitaji
uwepo wa utumishi wa umma uliotukuka unaozingatia utawala bora, utawala
wa sheria, maadili na mifumo thabiti ya usimamizi na utekelezaji.
Alisema
mipango na bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa ofisi hiyo imezingatia
dhamana hiyo ambayo imebeba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kuleta mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma kwa kuimarisha
uwajibikaji na uadilifu.
Alisema
utekelezaji wa dhamira hiyo utasaidia kujenga utumishi wa umma
uliotukuka kwa kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka, kuondokana na
ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuondokana na
ucheleweshaji wa maamuzi, kutosimamiwa kwa uwazi na kutowajibika kwa
viongozi na watumishi.
“Ni
lazima tuwe na viongozi wa umma wanaozingatia maadili yao ya kazi na
ndio maana tunasisitiza kuwa viongozi wote watakaobainika kuhusika na
ulipaji au kusaidia kulipa watumishi hewa mishahara, tutawafungulia kesi
za jinai,” alisema Kairuki.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene akiwasilisha hotuba ya bajeti
yake, alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, watumishi 78 wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa walichukuliwa hatua za kinidhamu na
kijinai.
Alisema
kati ya watumishi hao, ma-DED watano wamevuliwa madaraka na kupangiwa
kazi nyingine na wakurugenzi watatu wamefunguliwa kesi mahakamani na
kesi hizo bado zinaendelea.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment