John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Serikali imepangua uongozi wa vyombo vya dola mkoani Mwanza kwa
kuwahamisha vituo vya kazi watendaji wakuu akiwamo Kamanda wa Polisi,
Justus Kamugisha aliyehamishiwa mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa John
Mongella alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa taasisi hizo
na kukabiliana na matukio ya uhalifu yaliyotikisa mkoa huo tangu kuanza
kwa mwaka huu.
“Kwa
kipindi kifupi cha wiki mbili tangu nihamie
Mwanza, nimeshuhudia matukio kadhaa ya uhalifu, yakiwamo mawili ya
ujambazi yaliyoishia kwa raia wema kupoteza maisha na mamilioni ya fedha
kuporwa,” alisema Mongella.
“RPC amehamishiwa Mbeya ambako nadhani labda
kuna changamoto kidogo kulinganisha na zile za Mwanza alizoonyesha
kushindwa,” alisema Mongella.
Mongella alisema pamoja na RPC,
vigogo wengine waliohamishwa kutoka Mwanza ni pamoja na ofisa utumishi
wa jeshi la polisi, ofisa Idara ya Usalama wa Taifa na kamanda wa mkoa
wa Idara ya Uhamiaji.
Akizungumza na viongozi, watumishi na
watendaji wa vyombo vya dola wilayani Magu, Mongella aliwataka kutimiza
wajibu kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo
yao, akionya watakaoshindwa watawajibishwa.
“Haiwezekani
majambazi yatambe kwa kuvamia, kupora na kuua wananchi watakavyo, na
vyombo vya dola na viongozi wenye dhamana ya ulinzi na usalama wapo
wanashuhudia. Kila mtu atimize wajibu wake,” alisema Mongella.
Alitumia
fursa hiyo kuuagiza uongozi wa polisi wilaya ya Magu kukomesha matukio
ya mauaji ya kukata watu kwa mapanga yanayodaiwa kufanywa na watu
wanaokodishwa.
Ndani ya kipindi cha miezi miwili ya Februari na
Machi, Jiji la Mwanza limekumbwa na matukio sita ya ujambazi ambayo
yamechukua maisha ya watu sita waliouawa kwa kupigwa risasi, huku
mamilioni ya fedha yakiporwa kutoka maduka ya fedha kwa njia ya
mitandao.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment