Kisa Viatu Vipya, YONDANI ‘out’ YANGA SC

Mchezaji wa Yanga, Kelvin Yondani.
Dimbani leo kuvaana na Mwadui FC lakini imepata pigo la kuwakosa mabeki wake watatu wa kikosi cha kwanza akiwemo tegemeo wa kikosi hicho, Kelvin Yondani ambaye viatu vipya zimemsababishia matatizo.

Mbali na Yondani, mabeki wengine watakaoukosa mchezo huo ni beki wa kati, Mtogo, Vincent Bossou anayesumbuliwa na malaria yaliyomsababisha kushindwa kufanya mazoezi na wenzake jana na beki wa kushoto, Haji Mwinyi atakaa jukwaani kutokana na adhabu ya kadi tatu za njano alizonazo.

Kwa upande wa mastraika wapo sawa kasoro Matheo Simon, anayesumbuliwa na majeraha kidogo na anaweza kurejea uwanjani muda wowote.

Haijaishia hapo, kipa wa timu hiyo, Ally Mustapha ‘Barthez’ naye atakuwa nje kutokana na kuumia sehemu za mbavu katika mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri huku akitarajiwa kuanza mazoezi mwishoni mwa wiki hii.

Hao wote katika mazoezi yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar hawakuwepo kasoro Bossou aliyekuwa amepewa programu maalum ya kuzunguka uwanja muda wote bila ya kugusa mpira.
Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameliambia Championi Jumatano kuwa, Barthez ameshafanyiwa vipimo na ameonekana hana tatizo kwenye mbavu isipokuwa ni maumivu ya kawaida na mwisho wa wiki hii anaweza kuanza mazoezi taratibu.

Kuhusiana na Yondani, yeye alipata majeraha kwenye miguu yaliyosababishwa na viatu vipya alivyovivaa kwenye mechi yao dhidi ya Al Ahly wikiendi iliyopita na kuisha kwa sare ya 1-1 na mpaka jana Pluijm aliithibitishia Championi kuwa hana uhakika wa kumtumia katika mechi ya leo.
“Bossou yeye pamoja na kuja mazoezini lakini anaumwa malaria. Yondani pia amepata majeraha ya miguu kutokana na viatu vyake vipya alivyovitumia kwenye mechi iliyopita kwa hiyo sidhani kama watakuwepo kesho (leo) dhidi ya Mwadui.

“Alivaa viatu ambavyo ni vipya na ndivyo vilivyomuumiza.
“Barthez yeye amefanyiwa vipimo na ameonekana hakupata matatizo makubwa ila bado ana maumivu lakini mwisho wa wiki hii anaweza kuanza mazoezi na kikosi.

“Maandalizi yamekwenda vizuri, tumemaliza vizuri na nitakaa na wachezaji baadaye leo (jana) kuzungumza nao kwa ajili ya mechi ya Mwadui na kuangalia nani yupo fiti zaidi kwa ajili ya hiyo mechi, kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Pluijm.

Yanga imekutana na pigo hilo ikiwa kwenye harakati za kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya muda mrefu kiti hicho kushikiliwa na mahasimu wao, Simba SC.

Yanga pia inatarajia upinzani mkubwa kutoka katika kikosi hicho kinachonolewa na kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mwadui Compex, Shinyanga, iliisha kwa sare ya mabao 2-2.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment