Mbowe
aliitaja mikakati hiyo ikiwamo kamati za kuhamasisha Ukuta ambapo
aliyekuwa mgombea urais kupitia Ukawa Edward Lowassa amepangiwa Mbeya,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji atakuwa Mwanza, Makamu
Mwenyekiti Profesa Abdallah Safari atakuwa Tabora huku Mwenyekiti wa
Bawacha Taifa, Halima Mdee na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Mabere
Marando wakipangiwa Dar es Salaam.
Alisema
yeye (Mbowe) ataongoza Kanda ya Kaskazini wakati Profesa Mwesiga Baregu
amepewa jukumu la kufafanua Ukuta kwa taasisi za kimataifa, viongozi wa
dini na wastaafu.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu na mawakili 12 wao watajifungia Dar es Salaam kufungua kesi 21 kutetea mikutano.
Lakini, Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa rasmi baadaye huku CCM wakisisitiza msimamo wao wa kupinga maandamano hayo.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo litatoa
taarifa siku chache zijazo. “Tutawaita na tutazungumza, naomba tujaribu
tu kuvuta subira,”alijibu kwa ufupi msemaji huyo wa polisi.
Hata
hivyo kikosi cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika
mikoa mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam na Kilimanjaro walionekana
wakifanya mazoezi wakiwa na silaha na magari ya maji ya kuwasha kwa siku
tofauti.
CCM watoa ushauri
Msemaji
wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema licha ya chama kuzungumza mara
kadhaa, wanatarajia kutoa tamko kwa lengo la kuwaeleza Watanzania
tahadhari juu ya mchezo unaojaribiwa na Chadema.
Sendeka alisema viongozi wa dini na makundi mbalimbali yameshauri juu ya mipango yao, lakini hawataki kusikia.
“Jambo
hilo limezungumzwa mara nyingi sana, viongozi wa dini wameshasema, watu
wenye mapenzi na nchi yao wakishauri waache huo mchezo wao ambao
sidhani kama watafanikiwa, kwa hivyo tunatarajia kutoa tamko letu siku
yoyote kuanzia kesho (leo),”alisema.
Mbowe na safu yake
Akizungumza
wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini jana
katika Hoteli ya Coridol Springs jijini hapa, Mbowe alisema chama hicho
kimejipanga kufanya mikutano na maandamano ya amani nchi nzima Septemba
Mosi ili kutetea utawala wa sheria na Katiba.
Mbowe
alisema Rais Magufuli aliapa kuilinda Katiba, Wabunge waliapa kuilinda
Katiba, madiwani waliapa kuilinda Katiba ili nchi iongozwe katika
misingi ya sheria na utawala bora.
Alisema
haiwezekani nchi kuongozwa kwa matamko ambayo yanakiuka katiba na
Chadema kama chama kikuu cha upinzani kina wajibu wa kuishauri na
kuikosoa serikali na hawawezi kukaa kimya.
Alisema
matamko ya Rais kuwa hakuna ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa kwa
vyama vingine na kuacha chama chake kufanya mikutano na pia kuzuia
mikutano hadi mwaka 2020 haikubaliki.
“Sisi tunataka nchi iongozwe kwa kufuata sheria na siyo matakwa ya viongozi ambayo yanakinzana na sheria na Katiba ya nchi,” alisema Mbowe.
Alisema
wanafanya mikutano na maandamano kama sehemu ya kueleza malalamiko yao,
hasa kutokana na kauli za viongozi ambazo zinakiuka sheria.
Mbowe
alisema vyama vyote vikiamua kukaa kimya na kuacha mambo yaliyotokea
Zanzibar, yaliyotokea Dodoma na yanayotokea sasa kutokana na kauli za
viongozi, ni wazi nchi haitakuwa salama.
“Tukiamua
sote kujifanya wanafiki kusema hewala nchi haitakuwa salama itazaa
taifa la watu wenye hofu na ndiyo sababu tumeamua kamati kuu kuanzia
sasa kufanya kazi kila siku kuisaidia sekretarieti,” alisema.
Mbowe
alisema kutokana na unyeti wa Ukuta, Kamati Kuu ya Chadema imeunda
kamati ndogo tano, ambazo zitasaidia kufikiwa malengo yaliyokusudiwa kwa
kuhusisha taasisi na vyombo vingine.
Alisema
pia kuna kamati ya maandalizi ya Ukuta ambayo tayari imeanza kazi ya
kufafanua maamuzi ya kamati kuu, ambayo sasa imesambaa katika kanda zote
kutoa elimu kwa viongozi wa Chadema.
“Katika
kanda zote nchi nzima viongozi watakwenda kuzungumza na wanachama wa
kada zote na kuwaelimisha kwanini Kamati Kuu imefikia maamuzi ya
kuanzisha Ukuta kabla ya kushiriki mikutano na maandamano Septemba
Mosi,” alisema
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment