Janga la Watumishi Hewa: Waziri Asema Wameongezeka na Kufikia 16,127, Ripoti Rasmi Kukabidhiwa Kwa Rais Magufuli Agosti 26

TAARIFA rasmi ya mwisho ya utekelezaji wa kuwaondoa watumishi hewa serikalini na taasisi zake zote, itawasilishwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa wiki ijayo na kwamba hadi sasa wameshabainika watumishi hewa 16,127 na wameondolewa kwenye mfumo wa utumishi.

Aidha, mbali ya serikali kuokoa Sh bilioni 16.15 kwa mwezi huu wa Agosti baada ya watumishi hewa hao kuondolewa kwenye mfumo wa utumishi, ambao kama wasingeondolewa fedha hizo zilikuwa ziwalipe mshahara, posho na malipo mengine, waajiri 145 hawajawasilisha taarifa kuhusu uhakiki wao.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kuwataka waajiri wote wa umma na serikali, kuwaondoa watumishi hewa.

Akifafanua taarifa hiyo, Kairuki alisema Agosti 26, mwaka huu watamkabidhi rais taarifa rasmi ya utekelezaji wa agizo hilo huku akiwataka waajiri 145 ambao hawajawasilisha taarifa za ama uwepo wa watumishi hewa au la, kuhakikisha wanaziwasilisha taarifa hizo kabla ya Ijumaa wiki ijayo.

“Tunawapa muda hadi Ijumaa wiki ijayo wawe wamewasilisha taarifa za kama wana watumishi hewa au la na sisi Agosti 26, mwaka huu ndio tunamkabidhi rais taarifa rasmi ya mwisho ya utekelezaji wa agizo alilotoa,” alisema Kairuki akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kuagiza uhakiki huo Machi mwaka huu.

Akielezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa na waajiri hao, Kairuki alisema nchi ina jumla ya waajiri 409 wa serikali na taasisi mbalimbali za umma, na kati ya waajiri hao, hadi sasa waajiri 264 ndio waliowasilisha taarifa za utekelezaji wa agizo hilo.

Alisema kati ya waajiri hao 264 waliowasilisha, waajiri 63 wamethibitisha hawana watumishi hewa, huku waajiri 201 wakibaini uwepo wa watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.

“Tumepokea taarifa za utekelezaji wa agizo la rais alilitoa Machi 15, mwaka huu na hadi sasa waajiri 264 kati waliotekeleza agizo hilo, 201 wamebaini wana watumishi hewa,” alisema Kairuki.

Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa baada ya kufikia tarehe ya mwisho wa kupeleka taarifa hizo, Kairuki alisema jukumu lao ni kuzipokea na kukabidhi mamlaka ya uteuzi ambayo ndiyo iliagiza na ambayo ndiyo itaamua hatua za kuchukua.

Sambamba na hilo, Kairuki alisema hadi sasa jumla ya watumishi hewa 606, wameanza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo mashauri yao kupelekwa polisi na hivi sasa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), wanafanya uchunguzi na hatimaye watuhumiwa hao wafikishwe kwenye vyombo vya juu vya sheria.

Aidha, maofisa utumishi 233 waliohusika kwenye malipo ya mishahara hewa mashauri yao, wamefikishwa kwenye mamlaka husika kwa uchunguzi, ilhali watatu wamefukuzwa kazi, huku wizara ikiendelea kufanya uchunguzi kwenye taasisi 75 za umma ili kujiridhisha kuhusu suala la watumishi hewa.

Kuhusu waajiri 145 ambao hawajawasilisha taarifa za uhakiki wa watumishi wao, Kairuki alisema zimo taasisi, wakala, bodi, mabaraza, vyuo, hospitali, ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, tume na mamlaka kadhaa ambazo hazijawasilisha taarifa zao.

Kwa upande wa mabaraza nchini, Kairuki alisema mabaraza mbalimbali 10 hayajawasilisha taarifa za uhakiki wa watumishi na baadhi yao ni kama vile Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Baraza la Elimu ya Ufundi (Nacte), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Aidha, jumla ya vyuo vya umma 25 nchini havijawasilisha taarifa zao za uhakiki wa watumishi hewa na baadhi yao ni Dodoma (Udom), Chuo KIkuu Huria (OUT), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo cha Diplomasia, Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Upande wa Bodi mbalimbali ambazo hazijawasilisha taarifa zao jumla yake ni 10 na baadhi ya bodi hizo ni pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Bodi ya Utalii na Bodi ya Maziwa.

Pia zimo hospitali teule za rufaa tatu ambazo ni Hospitali ya CCBRT, Hospitali ya Rufaa Bugando na Hospitali ya Rufaa KCMC na kwamba katika hospitali kama hizo zilizowasilisha taarifa zake, wamebainika na kuondolewa watumishi hewa 4,000.

Kwenye taasisi za Umma na Wakala ambazo hazijawasilisha taarifa zao jumla ziko 30 na baadhi yao ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Makumbusho ya Taifa, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

Pia zipo Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12 ambazo baadhi yake ni Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dodoma, Dar es Salam, Mbeya, Pwani na Kagera; kwa upande wa mamlaka zipo sita ambazo ni Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Aidha, zipo tume 10 ambazo hazijawasilisha taarifa zake na baadhi yake ni Tume ya Pamoja ya Fedha, Tume ya Atomiki, Tume ya Elimu Taifa, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Pia zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 38 zikiwemo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Iringa, Nyamagana, Halmashauri ya Mji, Kasulu, Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment