AZAKI Yajitosa Mgogoro wa Zanzibar... Yataka Sherehe Za Mapinduzi Zitumike Kueleza Hatma Ya Kisiasa Zanzibar

 TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA TANZANIA (AZAKI) KUHUSU HALI YA KISIASA VISIWANI ZANZIBAR 10/1/2016
______________________________________
Sisi wana Asasi za Kiraia nchini - AZAKI, tulikutana tarehe 17 Novemba 2015, ambapo ni zaidi ya wiki tatu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika na kutathimini mwenendo wa uchaguzi mkuu na hali ya kisisasa visiwani Zanzibar.

 Baada ya tathmini yetu ya kina kama AZAKI tulitoa tamko na kuwataka wanasiasa kufanya mambo kadhaa ili kuinusuru Zanzibar na hali ya machafuko. 

Kati ya mambo tuliyowataka wanasiasa kuyazingatia ili kuendeleza amani na utengamano nchini ni pamoja na:
 
1. Uwepo utaratibu wa kutolewa taarifa ya maendeleo ya majadiliano yanayofanywa na viongozi wanaokutana kuhusu suala la muafaka wa kisiasa Zanzibar, ikieleza lengo la majadiliano na muda wake; ikumbukwe kikatiba, wananchi wana haki ya kujua na kushirikishwa katika masuala yoyote yanayohusu maslahi yao na nchi yao.
 
2. Wakati majadiliano yakiendelea, (i) Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kuwalinda wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi na kusiwe na utaratibu wa kuwanyanyasa kama inavyolalamikiwa na baadhi ya watu kuhusu manyanyaso yanayofanywa na wanausalama
 
3. Tuliwataka viongozi wanaojadiliana na wadau wengine wote wenye mchango katika kuiona Zanzibar inaishi kwa amani na salama, wajikite sana katika kuzingatia sheria na katiba wanapokusudia kufanya maamuzi ya utatuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar, kwa sababu kinyume na hivyo, watazua machafuko kwa kufikia maamuzi yasiyofuata au yanayokinzana na sheria na katiba. 

Kila mtu anawajibika kutii misingi ya sheria na katiba na pia masuala hayo ni muhimu katika kuepusha migongano na machafuko.

Baada ya Tamko hili AZAKI tumeendelea kufuatilia hali ya kisiasa Zanzibar. Tumefanya hivyo tukiamini kuwa uchaguzi ni sehemu muhimu ya michakato ya kidemokrasia hapa nchini kama ilivyo duniani kote.

 Sisi asasi za kiraia Tanzania, tukiwa watetezi na wasimamizi wa demokrasia, utawala bora na haki za binadamu, hatuegemei upande wa mgombea yeyote wala chama chochote cha siasa kinachotafuta kuingia madarakani wala hatulengi kuchukua dola bali tunataka haki itendeke Visiwani Zanzibar.

Aidha, AZAKI tunasikitishwa na hali isiyoridhisha ya kisiasa Visiwani humo ambayo imetokana na kufutwa kwa uchaguzi kwa sababu zisizokuwa na tija kwa taifa , uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. 

Tunaona kumeibuka mgogoro mkubwa wa kisiasa kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Bw. Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wote wa Zanzibar, kwa maana ya uchaguzi wa kumchagua Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar.

Tathmini yetu kama AZAKI tuliona uamuzi huo wa kufuta uchaguzi haukuwa sahihi kisheria na haukubaliki kwa sababu umevunja katiba na kwamba umefanywa kwa msukomo wa maslahi binafsi ya kisiasa kwa kuwa si Mwenyekiti wala Tume ya Uchaguzi yenye mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi. 

Kwa ufupi, hakuna kifungu chochote cha sheria wala Katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 kinachompa uwezo Mwenyekiti au Tume kuchukua uamuzi kama huo.

Uamuzi huo umezusha mtafaruku mkubwa huko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, umeibua malumbano na mivutano katika jamii na hiyo kwenda mbali zaidi kwa kuibua upya mvutano wa kisiasa kati ya vyama vikuu viwili vya siasa vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Hali ya Sasa ya Mazungungumzo
Huku tukitambua kwamba kukutana na kujadiliana kwa viongozi wa ngazi ya juu, wakiwemo marais wastaafu wa Zanzibar, ni njia muafaka ya kutafuta suluhu ya mgogoro, tunataka ieleweke wazi kuwa vikao visivyokuwa na mwisho wala taarifa inayotolewa kwa umma kuhusu maendeleo yake, havileti matumaini kwa wananchi. 

Ni haki ya msingi na ya kikatiba kwa wananchi kupewa taarifa ya maendeleo ya vikao hivyo; waelezwe vinalenga nini; na kwa muda gani viongozi wanaweza kumaliza majadiliano. 

Kwa mujibu wa Ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 kila raia anayo haki ya kupewa taarifa na kujua yote yote yale yahusuyo mustakabali wa taifa na maisha yake.

AZAKI tumebaini Mazungumzo ya viongozi wakuu yanafanyika katika hali ya usiri mkubwa na lililo baya zaidi hakuna utaratibu wa wananchi kupewa taarifa fafanuzi ya maendeleo ya mazungumzo hayo. 

Huku wanasiasa wa vyama hivo viwili wakisikika kutoa kauli zinazogonganisha wananchi na kuwachanganya. Matokeo yake kujenga hofu inayoumiza mioyo ya wananchi. 

Wananchi wananyimwa haki yao ya kujua masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yao hasa pale inapoonekana wazi walishiriki kupiga kura ya kuchagua viongozi wanaowataka. 

Hili limethibitishwa na asasi za kiraia za uangalizi wa uchaguzi za ndani ya nchi na hata waangalizi wa kimataifa.

Hofu kubwa tuliyonayo sisi wana Asasi za Kiraia ni kwamba kuendelea kwa ukimya mkubwa kunaongeza minong'ono katika jamii, hali inayoweza kuzusha migongano na kusababisha haki na amani kuchezewa na wasiokuwa na nia njema ya kuiona Zanzibar inaishi katika amani na kuendeleza utengamano kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). 

Kwa sasa kuna hali ya utata kuhusu uongozi uliopo madarakani Zanzibar kutokana na sababu mbalimbali za kisheria tulizoeleza katika tamko letu la awali.

Kwa mujibu wa Ibara ya 21 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ( kama ilivyoboreshwa mwaka 2010) kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shuguli za utawala kwa kupitia wawakilishi waliowachagua wenyewe. 

Katika mazingira ya uongozi wa Zanzibar yaliyopo kwa sasa, ni wazi kuwa nchi inaendeshwa kwa muda mrefu bila ya kuwepo chombo cha kutunga sheria na cha uwakilishi ambacho ni muhimili muhimu katika uendeshaji wa serikali. 

Katiba ya Zanzibar Ibara ya 90(1) imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW kwa muda usiozidi Siku Tisini (90) kuanzia Baraza lilipovunjwa.

 Kipindi hicho kikatiba kilikwisha toka tarehe 12 Novemba 2015, kwa kuwa Baraza lilivunjwa rasmi tarehe 13 Agosti 2015. Itakapofikia January 12/2016 itakuwa ni miezi miwili ziadi Zanzibar kuendeshwa bila uwepo wa Baraza la wawakilishi, kitu ambacho ni kinyume na Katiba.

Wito Wetu
1. Muungano wa Asasi za Kiraia Tz (AZAKI) tunatambua hatua busara za viongozi kutambua wajibu wao na kukutana kujadili njia ya kuondoa mgogoro. 

Tunadhani viongozi wamepata muda wa kutosha kujadiliana na sasa ni imani yetu kuwa wakati umefika kwa viongozi wanaokutana kutoka hadharani ikiwezekan siku ya maazimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, tena kwa pamoja, na kutoa taarifa fafanuzi inayojibu yafuatayo: 

Ajenda zao ni zipi? Wamefikia wapi? Wamebakiza wapi? Ni lini watamaliza majadiliano? Lini watatoa tamko la MUAFAKA wa kumaliza mgogoro?
 
2. Ni msimamo wa AZAKI kwamba katika hali yoyote ile, ni muhimu sana utatuzi wa mgogoro uwe unaozingati msingi wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Toleo la Mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya mwaka 1984. 

Tunasisitiza hili kwa kuamini kuwa upatikane uamuzi ambao utakubalika kisheria kwa maana ya kuwa hautafikiriwa kuhojiwa mbele ya sheria.
 
3. Tunawataka viongozi wote watumie siku ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwatangazia wananchi hatma ya Zanzibar kisiasa, kwa kuwa Mzanzibari anayohaki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika uamuzi juu ya mambo yanamhusu yeye na Taifa lake. 

Wananchi walishiriki kwa kupiga kura na sasa wanakila sababu ya kujua hatma ya viongozi waliowachagua. Haki hii ni ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 21 (2) ya Katiba ya Zanzibar, na inaweza kwenda kudaiwa mahakamani muda wowote.
 
4. Tunawasihi viongozi wote wa dini mbalimbali na wadau wa maendeleo kuingilia kati suala la Zanzibar kwani viashiria vya viongozi wakubwa kujibizana majukwaani vinaweza kuendelea kujenga chuki miongoni mwa jamii
 
5. Pia tunawakumbusha vyama vya siasa vyote viamke na kushinikiza Serikali ya Awamu ya Tano kulipatia ufumbuzi suala la Zanzibar ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.
 
6. Vile vile pande zinazohusika na mgogoro huu zijiepushe kutoa kauli za kuwachanganya wananchi, bali ni vyema taarifa zinazotolewa ziwe sahihi na zisiwe na mkanganyiko.
 
7. Wananchi nao ni wadau muhimu sana katika mgogogoro huu, kwani kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar Ibaara ya 9 (2) inaeleza wazi kwamba “ Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananch wenyewe”.

 Wananchi walishiriki kupiga kura ili kupata Serikali itokanayo na mamlaka yao, hivyo kitendo cha viongozi wachache kukataa uchaguzi na kutowapa taarifa za msingi kuhusu mkwamo huu wa Kisiasa ni kuvunja katiba ya Zanzibar.

 Kwa hali hii tunatoa wito, wananchi washirikishwe na kupewa taarifa zote za mkwamo huu wa kisiasa hatua kwa hatua. Hata hivyo tunapaswa kuwapongeza kwa ustahimilvu mkubwa waliounyesha na tunawasihi waendelee kuwa watulivu huku wakiendelea kudai haki yao na kutunza amani visiwani Zanzibar.
 
Mwisho
Sisi Asasi za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zilizoundwa na kutambulika kisheria na zinazofanya kazi katika masuala mbalimbali ya kisheria, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. 

Kwa umoja wetu tunasimamia na kuhimiza utawala wa sheria na haki za binadamu na masuala yote ya kimaendeleo ili kuhakikisha maisha ya watanzania yanakuwa bora katika nyanja zote. 

Kwa sababu hiyo, tunajiona tukiwa na jukumu kubwa la kukemea na kuvitaka vyombo husika kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka uvunjifu wa amani na hivyo kulinusuru Taifa letu.

Imetolewa kwa niaba ya AZAKI zote nchini na asasi miavuli zilizofanya Mkutano Jijijini Dar es Salaam Tarehe 10/1/2016
Kwa niaba ya Asasi zote, inaletwa kwenu na:

Ismail Suleiman
Katibu Mkuu- Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia (NACONGO)
Onesmo Ole Ngurumwa
Mratibu wa Kitaifa- Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Deus M Kibamba
Mwenyekiti -JUKWAA LA KATIBA TANZANIA
Martina Kabisama-Mratibu Taifa
Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini Mwa Afrika(SAHRINGON)
Stepheni Msechu
Mwakilishi- Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
Omary Said- Rais
Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS)
Salma Said
Mwenyekiti -Jumuiya ya Waandishi za Maendeleo Zanzibar- WAHAMAZA
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment