Meja Jenerali Msuya; Alivyokufa na Kufufuka -03

MEJA ALIYEKUFA (1)Meja Jenerali Msitaafu, Msuya
ILIPOISHIA… Siku ya Mei 10, tulirejea Tanzania na mara moja nikaenda kumwona daktari. Baada ya uchunguzi makini, daktari alipendekeza nikamwone mtaalam wa upasuaji ili aweze kuuondoa uvimbe mmoja kati ya ule niliokuwa nao  aupeleke Hospitali ya Muhimbili ili kufanyiwa uchunguzi. Nilipomwona Dk. Mlula ambaye alikuwa ni mtaalam wa magonjwa hayo, alinikagua uvimbe huo na akashauriana kwa kirefu na wataalam wengine. ENDELEA…
MEJA ALIYEKUFA (2)Akiwa hospitali
Akaniambia kwamba shingo huwa ina mishipa mingi ya fahamu na ya damu, hivyo kuifanyia upasuaji ni jambo linalohitaji umakini mkubwa.
Hivyo, alinishauri nipelekwe Hospitali ya Muhimbili ili nikafanyiwe kile kinachoitwa ‘Fine Needle Aspiration’ yaani utaalam wa kuchomeka sindano mahali penye uvimbe ili kujua chanzo cha uvimbe huo, badala ya kukata kipande cha nyama kwenda kukipima.
Siku iliyofuata nilikwenda Muhimbili na nikashuhudia jinsi kipimo hicho kinavyokuwa chenye kusababisha maumivu makali kwa mhusika.  Hapakuwa na unafuu wowote kama neno ‘fine’ linavyotumika katika kipimo hicho. Mchakato mzima ni wa mateso makubwa ambapo mke wangu hakuvumilia kuona jinsi sindano ilivyokuwa inachomekwa katika shingo yangu kila mara ikiwa na kidude kilichoitwa ‘bunduki ya sindano’ kilichotumika kunyonya vitu kutoka shingoni.
meja
Alivyo sasa
Sindano hiyo ilikuwa inaingia na kutoka katika mwili wangu kama vile cherehani inavyoshona nguo. Mara moja aliondoka katika chumba hicho ili asizimie. Mtaalam aliyeendesha kipimo hicho alipata vitu kadhaa alivyotegemea lakini aliona havitoshi. Hivyo, aligeukia upande wa pili wa shingo na kurudia mchakato uleule.
Baada ya wiki moja, matokeo yalitolewa kwamba uvimbe huo ulikuwa haujulikani chanzo chake, kwa hiyo hapakuwa na haja ya kufanya uchunguzi au tiba zaidi. Kiukweli, sikumwamini mtaalam huyo aliyefanya kipimo hicho. Hakuniridisha kwamba alikuwa ni mtaalam makini wa kazi yake.

Siku moja wiki hiyohiyo, nilijikuta natapika kwa kiasi kikubwa wakati wa jioni na usiku wake. Nilimpigia simu daktari wangu ambaye alinishauri kunywa maji mengi na kumwona asubuhi iliyofuata hospitalini. Hadi nilipokwenda kumuona asubuhi, nilikuwa najisikia vibaya sana. Mara moja aliamua nilazwe hospitalini ili niweze kuongezwa maji mwilini kukwepa uwezekano wa kuishiwa maji.

Mipango yote ya kulazwa ikafanywa, manesi wakanipima shinikizo la damu, kiwango cha sukari na mkojo, ambapo pamoja na hayo, waliniwekea dripu. Wakati huo ilikuwa ni saa nne asubuhi.
Habari zikaenea kwamba nilikuwa mgonjwa sana na nilikuwa nimelazwa hospitalini, hivyo, kama kawaida, watu walianza kufika hospitalini hapo. Hadi kufikia adhuhuri, watu walikuwa wamejazana kwa wingi mno, kiasi kwamba walikuwa wanaruhusiwa kwa mafungu kuja kuniona. Nilijisikia faraja kubwa sana moyoni kutambua na kuliona jambo hilo.
Manesi walianza kuona hali inakuwa ya vurugu, hivyo wakaamua kuwaomba watu waliokuja kuniona waondoke ili waweze kupata nafasi ya kufuatilia hali yangu na kuruhusu watu wengine waliokuwa wakija waweze kuniona kwa muda mfupi. Hali iliendelea hivyo kwa siku nzima.

Jioni, kunako saa moja, nilihisi kutamani kitu kama chungwa au kitu fulani kitamu ili nile; hivyo nilimwomba mke wangu anikatie chungwa moja. Alichukua moja na kunikatia. Kwa mshangao wa kila mtu, sikuweza kulipeleka chungwa hilo mdomoni mwangu, badala yake nilianza kuhema kwa kukosa hewa na kwa mshangao wa kila mtu, nilizimia.
Watu waliokuwepo wakashikwa na hofu kubwa. Mtu mmoja akawaita haraka manesi ambao nao walikuja mbio kwa hofu kwa vile jenerali ambaye alikuwa bado ana nguvu zake ghafla alikuwa amezimia. Walihisi kwamba huenda kiwango cha sukari mwilini mwangu kilikuwa kimeshuka na kusababisha matatizo hayo.

Hivyo, walifanya vipimo haraka na kuthibitisha hilo ambapo walinipa vipimo viwili vya dripu ya ‘glucose’ na wakaongeza viwili katika chupa ya maji ya chumvi ambayo ilikuwa inaendelea kuingia katika mkono wangu. Katika muda wa dakika chache niliamka na kushangaa ni nini kilikuwa kimenitokea. Niliomba nisindikizwe msalani nikiwa bado na vidude vya dawa ya dripu vikiwa mwilini.
Mke wangu alikibeba chuma cha kushikilia vifaa vya dripu ambapo kwa pamoja tulitembea kuelekea bafuni kama tulivyokuwa siku ya kufunga ndoa.
Kunako saa sita za usiku wageni wote walikuwa wameondoka. Ni mke wangu na binti wa shemeji yangu wa kike aitwaye Evelyne, ndiyo waliobaki kunihudumia. Baada ya muda, wote tulilala. Saa tisa za usiku, kiwango cha sukari kilishuka tena, wakati huo nikiwa usingizini. Kilichowaamsha mke wangu na binti yangu ni kelele za kuhema nilizokuwa ninazifanya.

Nilifanya kelele kama zinazofanywa na ng’ombe wakati akichinjwa, ambapo mate mazito yalikuwa yakichuruzika kutoka mdomoni. Nilikuwa naelekea katika mauti.
Mke wangu alipokwenda kuwaita manesi waliokuwa zamu, alishangaa kugundua kwamba hapakuwepo na nesi yeyote. Walikuwa wamekwenda pasipojulikana. Kwa bahati, nesi mmoja alitokea. Kwa vile idara ile ilikuwa haimruhusu, hakuweza kufahamu glucose ilikuwa inahifadhiwa wapi, hivyo alilazimika kukimbia kwenda idara ya wagonjwa wa nje ambako aliipata na kuharakisha sehemu nilikokuwa natibiwa, yaani sehemu ya watu mashuhuri, alinikuta bado nimezimia ambapo binti yangu alikuwa akiniinua mgongoni na mke wangu akinipangusa usoni na taulo lenye maji.

Nesi huyo aliniwekea dozi mbili za dripu ya glucose, ambapo mwili wangu ulitulia ukaacha kutetemeka na kuhema, ambapo baada ya dakika kama kumi hivi, nilizinduka, fahamu zikanirudia nikijihisi na kuonekana kama mzuka.
Wakati huo Mungu Mwenyezi alinipa ushuhuda mwingine. Aliniokoa kutoka karibu na kifo; si kwa nguvu au uwezo bali kwa upendo wake. Jina lake litukuzwe. Asubuhi madaktari walikuja kuniona na kunipa pole kwa kilichotokea. Msimamizi wa hospitali alikuwa nao na alisikia kilichotokea.
Kulikuwa kumetokea uzembe kwa upande wa manesi kwani baada ya tukio la kwanza la kushuka kwa sukari wasingeondoka karibu ya kitanda changu.
Je, kiliendelea nini? Fuatilia mtandao huu wa tanzanialeo.com siku ya Jumatano.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment