Mkuu wa Mkoa Anne Kilango Malecela Atema Cheche Kufuatia Maagizo ya Rais MAGUFULI

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ametoa siku sita kwa Wakurugenzi wa Halmashauri tatu za Ushetu, Msalala na Kahama zilizopo wilayani Kahama kuhakikisha wanawakilisha kwake majina ya watumishi hewa ifikapo Jumatano ijayo.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa halmashuri zote tatu za Wilaya ya Kahama muda mfupi baada ya kumaliza ziara yake ya siku moja ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Kahama, ikiwa ni sambamba na kuwapa pole waathirika wa mvua kubwa ya mawe katika kijiji na Kata ya Mwakata.

Mvua hiyo ya mwanzoni mwa Machi mwaka jana ilisababisha maafa makubwa, ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 38 na kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Kilango alisema lundo la watumishi hewa katika halmashauri hizo halikubaliki, hivyo ni wajibu wa wakurugenzi kuhakikisha kuwa majina yao yanawakilishwa ofisi ya mkuu wa mkoa sambamba na maelezo ya kumbukumbu zao za ajira, wanavyolipwa na kiasi wanacholipwa.

“Hata wakurugenzi wakiwaficha, tayari orodha yao ninayo mezani…naomba mniletee majina,” alisema mkuu huyo wa mkoa aliyeanza kazi hivi karibuni baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli.

Katika Awamu iliyopita ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Anne Kilango alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Pia aliwataka viongozi wa halmashauri hizo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kukusanya mapato, ikiwa ni sambamba na kuongeza weledi ili mapato hayo yasipotee.
“Maendeleo ya Kahama yanatuhusu wote. Sipendi kumsimamisha mtu kazi kwa tuhuma za ubadhirifu, lakini ikibidi kufanya hivyo nitafanya kulingana na kasi ya uongozi wa Serikali ya Awamu Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli,” alisema.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment