Wachezaji wa Stand United
Ibrahim Mussa, Dar es SalaamSHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeshtushwa na matokeo ya mchezo wa kupata bingwa wa Mkoa wa Katavi baada ya timu ya Stand FC kuibuka na ushindi wa mabao 16-0 dhidi ya Kamazima hali ambayo TFF imekiagiza Chama cha Soka Mkoa wa Katavi (KRFA) kufanya uchunguzi wa matokeo hayo.
Mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi, ulikuwa ni wa kumpata bingwa atakayeuwakilisha mkoa huo kwenye Ligi ya Mabingwa Mkoa ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Kabla ya mchezo huo wa mwisho, timu ya Nyundo FC ilikuwa inaongoza kwa kuwa na pointi 21 na mabao 24 ya kufunga, ambapo Stand FC ilikuwa ikihitaji ushindi wa mabao 13-0 ili kuweza kuwa bingwa wa mkoa huo.
Taarifa iliyotumwa jana na TFF, imesema: “Baada ya Stand kushinda kwa mabao 16-0, inaonyesha kuna dalili za upangaji wa matokeo, hivyo KRFA haitaruhusiwa kutangaza bingwa wa mkoa huo hadi uchunguzi utakapokamilika na TFF ijiridhishe na uchunguzi huo.”
Ikumbukwe kuwa, hivi karibuni TFF ilizuia kuitangaza timu iliyopanda daraja kutoka Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuhisi kuwepo kwa vitendo kama hivyo ambapo katika mechi za mwisho, Geita Gold Sport iliifunga JKT Kanembwa mabao 8-0, huku Polisi Tabora ikiinyuka JKT Oljoro mabao 7-0.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment