Tajiri Aliyedaiwa Kuua Kwa Risasi, Mazito Tena!

IMG_0674David Kalangula enzi za uhai wake.
Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI DAR ES SALAAM: Mazito yameibuka kuhusu bosi wa Kampuni ya Tripple A Hauliers inayosafirisha petroli mikoani na nje ya nchi, Hussein Jeta (30), ambaye alikamatwa kwa madai ya kumuua kwa risasi dereva wake, David Kalangula (36), baadaye kusemekana aliachiwa. 

Tukio hilo lilitokea Oktoba 19, mwaka jana,  Mbagala Mission, Dar ambapo bosi huyo alishikiliwa Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke, baadaye akapelekwa Mahakama ya Wilaya ya Temeke na kuachiwa huku ikidaiwa amekimbilia nchini Canada. 

Taarifa mpya kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Gilles Muroto ni kuwa, amefuatilia suala hilo kwa upande wa jeshi la polisi mkoani mwake na kubaini hakuna njama zozote zilizofanyika ili mtuhumiwa huyo aachiwe huru na mahakama akiwa mahabusu Gereza la Keko, Dar.
Kamanda Muroto aliendelea kusema:
IMG_1921 
Mke wa marehemu.
“Watu wa kubanwa ili kujua jinsi Jeta alivyoachiwa huru ni Mahakama ya Wilaya ya Temeke, wao ndiyo walitoa amri ya kuachiwa na si polisi.
“Hata aliyedaiwa kuwa ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke (RCO), aliyetajwa kwa jina la Rashid kwamba aliandika barua, jina hilo halipo na aliyopo amekataa kuandika barua hata sahihi si yake.”
Kuachiwa huru kwa Jeta kwa amri ya mahakama, kumewatia shaka wananchi wanaofuatilia taarifa hiyo, wengi wakijiuliza kwa nini Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Harrison Mwakyembe amekaa kimya!

“Jamani, hii habari ya Jeta kuachiwa huru niliisoma kwa mara ya kwanza kwenye gazeti lenu la Uwazi, kwamba alidaiwa kumuua dereva wake. Pia nikaja kusoma amechiwa huru na mahakama. Sasa hizi habari kwani waziri wa sheria, Mwakyembe yeye hazisomi? Kama anasoma mbona anakaa kimya?” alihoji Julius Mtalilo, mkazi wa Mbagala, Dar.

Taarifa zilizopatikana awali kutoka kwa baadhi ya polisi wa Kituo cha Chang’ombe ambao walimshikilia mtuhumiwa, inadaiwa Jeta aliachiwa huru Desemba 7, mwaka jana.
Lakini mbali na madai kuwa amekimbilia Canada, habari za karibuni zinasema hata mkewe na mtoto wao mmoja hawapo nchini.
IMG_1919 
Mke wa marehemu akiwa na watoto wake.
Uwazi katikati ya wiki iliyopita, lilifika nyumbani kwa familia hiyo, Upanga, Dar na kukuta mlango umefungwa ambapo baadhi ya majirani walipoulizwa walisema hawajui lolote.
Jeta alikamatwa na mwenzake aitwaye Ali Bimji (27), ambapo kesi yao ilifikishwa Mahakama ya Wilaya Temeke na kupewa namba P1 7/2015 kisha wote walipelekwa Keko, Novemba 2, mwaka jana.

Kwa mujibu wa askari wa Chang’ombe, upelelezi wa awali ulimtia hatiani Bimji kwa vile ndiye mmiliki wa bastola lakini siku ya tukio, Jeta alimnyang’anya na kudaiwa kuitumia kumpiga risasi mbili David.

Marehemu David alidaiwa kupigwa risasi katika ofisi za kampuni hiyo muda mfupi baada ya kurejea kutoka safarini na kutoa taarifa ya upotevu wa mafuta ndipo kukawa na malumbano na bosi wake huyo na baadaye kupigwa risasi.
naMkuu wa jeshi la polisi, IGP Mangu.
Oliver Donatus Msola ni mke wa marehemu David, yeye alizungumza na Uwazi, Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Kibamba, Dar na kusema kuwa wanaitegemea mahakama kutenda haki katika kesi hiyo.
Alisema kwa upande wa huduma kutoka katika kampuni hiyo, kuna mkataba ambao hajausaini ukionesha kuwa atapewa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuanzisha biashara. Pia alisema kampuni hiyo imejitolea kuwasomesha watoto wote (watatu) wa marehemu hadi ukomo wa elimu yao.

Alhamisi iliyopita, Uwazi lilifika mahakamani Temeke lakini waandishi wetu walinyimwa ushirikiano kuhusu kutajiwa hakimu aliyetoa amri ya Jeta aachiwe.
Pia, juzi mchana, Uwazi lilimpigia simu Waziri Mwakyembe ili kumsikia anasemaje kuhusu hali hiyo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
-GPL
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment