Uganda Yaridhika Bomba la Mafuta kuishia Bandari Ya Tanga

WAZIRI wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni amesema ameridhishwa na eneo lililotengwa kwa ajili ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert hadi Bandari ya Tanga.

Alitoa kauli hiyo jana alipoongoza ujumbe wa wataalamu na wawekezaji kutoka mashirika ya TOTAL, TULLOY na CNOOC ambayo yanatarajiwa kutekeleza ujenzi wa mradi huo; na kutembelea maeneo utakapojengwa mradi wa bomba la mafuta ghafi katika Bandari ya Tanga.

Muloni alisema baada ya kupata maelezo ya kina na kutembelea Bandari ya Tanga ameridhishwa na mazingira yaliyopo na kwamba wiki ijayo Serikali ya Uganda itatuma timu ya wataalamu watakaokagua maeneo yote yatakapopita mabomba na ujenzi wa matangi ya kuhifadhia ili kujionea hali halisi kabla ya kuruhusu mradi kuanza kutekelezwa.

“Nimeona taarifa ya mradi iliyowasilishwa hapa na wataalamu na pia nimepata fursa ya kutembelea Bandari ya Tanga na kimsingi nimeridhika na wiki ijayo nitatuma timu ya wataalamu ili kuja kufanya uhakiki na kushauri kabla ya utekelezaji rasmi kuanza,” alisema Muloni.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Justin Ntalikwa alisema amefurahishwa na ujio wa ujumbe huo ambao utarahisisha uamuzi wa kujengwa mradi huo nchini hasa baada Serikali ya Kenya kuanza kushawishi mradi huo ufanyike nchini humo.

“Tumethibitisha kwamba kupitia bandari hii ya Tanga tunavyo vigezo vya kuweza kutekeleza mradi huu hasa ikizingatiwa kwamba tunao mtandao mzuri wa miundombinu ya reli, barabara na bandari ambayo hata mradi utakapoanza tutaweza kuleta vifaa kwa urahisi tofauti na wenzetu wa nchini Kenya,” alisema Ntalikwa.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Matarajio alisema mazingira ya Bandari ya Tanga ambayo inazungukwa na visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na vingine ni salama zaidi kwa meli kufanya shughuli zake bila kukumbwa na hatari ya mawimbi makubwa ya bahari.

“Bandari ya Tanga ni tofauti kabisa na bandari nyingine ambazo zimekwisha tembelewa kama bandari ya Lamu ya nchini Kenya ambayo haifanyi kazi. Kwanza ina kina kirefu sana cha zaidi ya mita 40 wakati meli kubwa kama hizo za mafuta zinahitaji kina cha mita 18 na vile vile Bandari ya Tanga imeunganishwa na mtandao wa barabara na reli ambao unaweza kusafirisha mizigo hapa ukaipeleka Dodoma, Mwanza, Burundi hadi Uganda.

“Hivyo tunatumaini kwamba Serikali ya Uganda itakapokuwa inafanya maamuzi yake itachukua ruti ya Tanzania kama ambavyo viongozi wetu wa nchi walisaini makubaliano ya kuutekeleza huu mradi,” alisema Dk Mataragio.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema mkoa huo umejipanga kupokea mradi huo na ambao utaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanga na Taifa.

Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi unatarajiwa kujengwa katika eneo lililopo kati ya visiwa vidogo vya Fungunyama, Ulenge na Chongoleani jijini Tanga na unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni nne hadi kukamilika.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment