Kikosi kazi maalumu cha kuchunguza makosa makubwa ya kihalifu kimewatia
mbaroni vigogo wawili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakihusishwa na
utoaji wa kibali cha kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.
Maofisa
hao ni Mkurugenzi wa Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Dk
Charles Mulokozi na ofisa mfawidhi wa kituo cha uwindaji wa kitalii,
utalii wa picha na Sites cha jijini Arusha, Nyangabo Musika.
Kikosi
hicho kinaundwa na wachunguzi kutoka Polisi, Idara ya Uhamiaji, Usalama
wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kikosi cha kupambana
na ujangili nchini na Takukuru.
Wakati Dk Mulokozi anakamatwa,
tayari alikuwa amesimamishwa kazi kwa agizo la Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kutoa kibali wakati Serikali
ilishazuia.
Vyanzo mbalimbali vimesema jana kuwa
Dk Mulokozi alikamatwa mwishoni mwa wiki na jana alisafirishwa chini ya
ulinzi kwenda kituo cha polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (Kia).
“Hivi
tunavyozungumza, Dk Mulokozi yuko njiani anapelekwa Kia chini ya ulinzi
mkali wa polisi.Nyangabo yeye tayari yuko mikononi mwa vyombo vya
ulinzi na usalama pale Kia,” kilidokeza chanzo chetu cha uhakika.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alipoulizwa jana
hakukanusha wala kukiri kuwa na taarifa za kukamatwa vigogo hao, lakini
alisema atakuwa na mamlaka ya kuliongelea wakiingia mkoani kwake.
“Bado
sijapewa hizo taarifa, lakini hata kama ningezijua nisingeweza
kuzungumzia tukio la kukamatwa kwao lililofanyika mkoa mwingine.
Nikikabidhiwa ndiyo naweza kusema chochote,” alisema Kamanda
huyo.
Hata hivyo, Waziri Maghembe alithibitisha kukamatwa kwa
vigogo hao, akisema katika tukio hilo yeyote aliyetia mkono wake lazima
akamatwe na kushitakiwa.
“Ni kweli Dk Mulokozi amekamatwa na
siyo yeye tu kuna ofisa mwingine pale ofisi yetu ya Arusha naye
tumemkamata. Hatuna mchezo katika suala hili,” alisisitiza.
Profesa
Maghembe alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa raia wa Uholanzi
waliokamatwa na polisi hawakuwa na vibali halali vya kufanya biashara ya
kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi kama baadhi ya watu
wanavyodai.
“Hawa Waholanzi walikuwa na tourist visa (waliingia
kama watalii). Halafu Watanzania waelewe mtu hawezi kupata kibali cha
kusafirisha mnyama hai kabla ya kumkamata, kuhesabiwa, akakaguliwa na
kupata vibali stahiki,” alisisitiza.
Raia hao wa kigeni
ambao ni ndugu wa familia moja, Artem Alik Vardanyian (52) ni mkurugenzi
wa mgahawa huko Uholanzi na Eduard Alik Vardanyian (44), meneja wa
hoteli huko huko Uholanzi.
Hata hivyo, vyanzo vingine
vimedai kuwa pamoja na kuwapo kwa vibali hivyo, lakini
hapakuwapo na “release order” inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), kama sheria inavyoelekeza.
Chanzo hicho kilidai wanyama
hao walikuwa wasafirishwe kwa kutumia ndege ya mizigo ya kukodi ambayo
ilitokea Afrika Kusini na ilikuwa iwapeleke wanyama hao Albania kupitia
Nairobi nchini Kenya na Nigeria.
“Hao marubani wa hiyo ndege
waliitwa pale Polisi (Kia), wakaandikisha maelezo yao kuwa walikuja
kuchukua wanyama hao na wakaambiwa wao waondoke tu hakuna mnyama
anaondoka,” alidokeza ofisa mmoja katika uwanja wa Kia.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment