Bajeti 2016/2017 Kuanza Kuchambuliwa Leo

Kama za Kudumu za Kisekta leo zinatarajia kuanza kuchambua taarifa za utekelezaji wa Bajeti za Wizara zinazosimamiwa na kamati hizo.
Hatua hiyo inafanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 98 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Akizungumza jana Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya alisema kwa takribani siku tisa Kamati za Kisekta zitakuwa na kazi ya kuchambua na kuangalia kama vipaumbele vimezingatiwa katika bajeti ya wizara husika.

Mwandumbya alisema katika kipindi hicho, Kamati ya Bajeti itafanya uchambuzi wa Mapendekezo ya Mpango na kiwango cha ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

“Kamati zina mamlaka ya kuhamisha kasma moja kwenda nyingine, na kama inaona kuna haja ya kupunguza au kuongeza bajeti ya wizara husika basi mapendekezo hayo yanapelekwa kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itashauriana na Serikali,” alisema.

Mwandumbya alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 98(3) ya Kanuni za Bunge, Aprili 15, mwaka huu kutakuwa na kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti ili kujadili mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye Kamati za Kisekta wakati wa kujadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara mbalimbali.

Juzi Serikali iliwasilisha mbele ya wabunge wote Mapendekezo ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2016/2017 inayotarajiwa kuwa ya Sh trilioni 29.539.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment