Hakimu FEKI Atiwa Mbaroni Mwanza

Mkazi  wa kijiji cha Kanyama Kata ya Bujora Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Erick Mkundi (23), ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya kazi kama Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kongoro akiwa hana sifa hiyo.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuifanya kazi hiyo kuanzia Januari hadi Aprili 6, mwaka huu alipobainika baada ya kushindwa kujitambulisha kwa Hakimu Mfawidhi wa wilaya hiyo, Edmund Kente, kuwa ni hakimu na bila kuonyesha nyaraka zozote zinazomthibitisha kuwa  na taaluma hiyo.

Aidha, ilidaiwa kuwa Mkundi alijikabidhi katika mahakama hiyo na kuanza kuendesha kesi na hadi anatiwa mbaroni, tayari alishatoa hukumu kwa washtakiwa wanne na wengine kadhaa kuwasotesha mahabusu.

Akizungumza jana, mmoja wa watumishi wa mahakama hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa madai kuwa si msemaji, alieleza kuwa walifanya kazi na Mkundi kwa miezi minne wakiamini kwamba ni mtumishi halali wa Idara ya Mahakama.
“Mkundi tuliamini ni hakimu halali, kwani alikuwa akiletwa na gari kama mheshimiwa fulani hivi, lakini baada ya kukamatwa Aprili 7, mwaka huu, ndipo tulipogundua ni mfanyakazi ‘hewa’, alisema mtoa taarifa huyo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Magu, Charles Mkapa, alisema Mkundi alikamatwa baada ya polisi kupewa taarifa zake za kufanya kazi bila kibali.
“Kweli tunamshikilia Mkundi tangu Aprili 7, mwaka huu, kwa tuhuma hizo, lakini taarifa kamili mnaweza kuzipata kwa Hakimu wa Wilaya ya Magu, kazi yetu ilikuwa kumtia mikononi mwa polisi,” alisema Kamanda Mkapa.

Awali, ilisemekana mtuhumiwa huyo aligundulika kuwa ‘feki’ baada ya kushindwa kulipa Sh. 40,000 yakiwa ni malipo ya gari alilokodi kwa ajili ya kutembelea kwenda na kurudi kazini pamoja na maeneo mbalimbali.

Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa Mkundi baada ya kushindwa kulipa gharama hizo, mmiliki wa gari alitoa taarifa kwa bosi wake wilayani na ndipo alipoanza kufuatiliwa.

Aidha, Mkundi ilidaiwa alikuwa akipokea rushwa na zawadi mbalimbali kutoka kwa watu aliokuwa akiwahudumia kimahakama, zikiwamo mbuzi pamoja na fedha kwa lengo la kusimamia kwa ukaribu tuhuma zinazowakabili.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe, alipoulizwa kuhusiana na tukio la ‘hakimu huyo feki’, alisema hajapata taarifa kamili, lakini atalizungumzia suala hilo leo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment