Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Edwin Amandus Ngonyani.
Elvan Stambuli na Sifaeli PaulNaibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Edwin Amandus Ngonyani (MB) amesema serikali haitaongeza hata siku moja terehe ikifika ya kuzima simu feki.
Katika mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni, Naibu Waziri Ngonyani alijibu maswali mengi, ungana nasi ili kujua mengi:
Swali: Unasimamia wizara tatu zilizounganishwa pamoja, ni changamoto gani mnazokumbana nazo?
Jibu: Hadi sasa naweza kusema hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza katika usimamiaji wa wizara hii ambayo ni zao la wizara mbili (Wizara ya Ujenzi; na Wizara ya Uchukuzi) pamoja na Idara mbili za sekta ya mawasiliano kutoka iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano Sayansi na Teknolojia. Wizara hii ina jumla ya taasisi zipatazo 26.
Kama wizara tumejipanga vema kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini kuhakikisha tunatimiza lengo kuu la kuwajengea Watanzania miundombinu ya kisiasa itakayowezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Tulianza na kukutana na menejimenti ya taasisi hizo zilizopo chini ya wizara pamoja na watumishi wa wizara ili kuainisha changamoto zinazowakabili ambazo katika changamoto hizo zilionekana zinaweza kutatuliwa endapo kila mtumishi atajituma na kuwajibika katika eneo lake. Tuliwaeleza watumishi hao kuwa kila mmoja atapewa malengo na atapimwa kulingana na malengo aliyopewa.
Mambo mengine tuliyowakumbusha ni ushirikiano baina ya watumishi wa sekta hizo ili kuiwezesha wizara kufanya kazi kama timu moja; uadilifu na uaminifu katika kazi; kuwa makini katika kuingia mikataba; na kusimamia utekelezaji wa mikataba tunayoingia kwa weledi wa hali ya juu ili Watanzania wapate thamani ya fedha yao wanayoilipia (value for money).
Swali: Hivi sasa kuna mjadala juu ya kuzima simu zote feki ifikapo Juni, mwaka huu kama wizara, mnalizungumziaje hili? Je, nani wa kulaumiwa kufuatia kuzagaa kwa simu feki nchini? Je, mtaweza kusogeza mbele tarehe ya kuzizima simu hizo?
Jibu: Vifaa vya mawasiliano vya mkononi-hususan simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) vina namba maalum inayovitambulisha. Namba hiyo inajulikana kama IMEI ambacho ni kifupi cha International Mobile Equipment Identity.
Kifungu cha 84 cha sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka kuwepo kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi. Rajisi hii inajulikana kwa Kiingereza kama Central Equipment Identification Register, kwa kifupi CEIR. Sheria inataka rajisi hiyo ihifadhiwe na kuendeshwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Aidha, kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta za namba tambulishi za mwaka 2011 za EPOCA kuhusu Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi inawataka watoa huduma wa mawasiliano yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi yaani Equipment Identity Register – EIR za vifaa vya mkononi vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Mfumo huu wa kielektroniki ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza kufanya kazi kwenye mitandao ya mawasiliano kutumia vifaa vya mkononi.
Mtu yeyote ambaye atatambua kwamba simu yake ya kiganjani si halisi baada ya kuihakiki kwa kuandika namba *#06# na kuituma kwenda 15090 na kugundua ni bandia na haikidhi viwango anapewa muda wa kuendelea kutumia simu hiyo hadi Juni 16, mwaka huu. Watumiaji wote wenye simu za kiganjani ambazo namba tambulishi zao zinaonesha kwamba simu hizo si halisi, ni feki na hazikidhi viwango watagharamia ununuzi wa simu nyingine wao wenyewe. Hatutaongeza hata siku moja kuzima siku feki.
Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano kupitia Kanuni za Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Simu za Kiganjani (Central Equipment
Identification Register-CEIR) kuwa mfumo huu uanze kazi haraka iwezekanavyo. Tayari Mfumo huu umeanza kazi tangu tarehe 17 Desemba 2015 baada ya kuzinduliwa na Katibu Mkuu Kiongozi.
TCRA ilitoa miezi sita hadi kufikia tarehe 16 Juni 2016 simu zote ziwe zimefungwa. Naomba kuchukua fursa hii kusisitiza Mamlaka ya Mawasiliano ihakikishe kuwa zoezi hili la kufungia simu bandia linatekelezwa kama ilivyoagizwa na viongozi wa Kitaifa bila kuongeza muda wa kusubiri ambao hawatakuwa wamekamilisha kuhakiki na kufahamu kama simu zao ni bandia au la.
Ningependa vilevile kuwasisitizia kampuni zote za simu kutoa ushirikiano wa dhati ili kukamilisha zoezi hili. Aidha, naelekeza makampuni hayo kuwapa huduma stahiki bila usumbufu wateja wao waliopotelewa au kuibiwa simu zao na zifungwe kwa mujibu wa kanuni ili zisiweze kufanya kazi. Hali kadhalika, niwaombe jeshi la polisi kuwasaidia raia watakaofika kutoa taarifa za kuibiwa au kupotelewa simu zao, wawape ushirikiano na kuwahudumia kwa haraka ili zoezi hili lifanyike kwa mujibu wa sheria na kanuni zake.
Hakuna mtu wa kulaumiwa katika hili kwani hii ni moja ya changamoto ambayo inazikabili nchi nyingi duniani ikiwa ni pamoja na kuwepo bidhaa nyingi feki katika nchi nyingi, zikiwemo bidhaa za ujenzi, madawa nk ambavyo huingizwi nchini na wahalifu kupitia njia za panya.
Mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tablets). Uanzishwaji wake ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010. Ni vyema watumiaji wakazingatia maelekezo kuhusu utaratibu wa kuhakiki namba tambulishi, kutoa taarifa wanapopoteza au kuibiwa simu.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment