Ofisa wa TRA na Mfanyakazi Mmoja wa Yono Auction Mart Wafikishwa Mahakamani Kwa Rushwa


Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Mkwizu na mfanyakazi wa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Edward Magobela wamepandishwa kortini jana wakikabiliwa na mashtaka matatu ya rushwa. 

 

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh50 milioni na nyingine ya Sh5 milioni na kupokea Sh3 milioni kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Commercial Sales and  Services Tanzania Limited, Glenn Clarke. 

 

Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lekayo alidai washtakiwa hao waliomba na kupokea kiasi hicho cha fedha ili kumwezesha mkurugenzi huyo kupunguziwa kodi aliyokuwa anadaiwa kutoka Sh375 milioni hadi Sh100 milion. 

 

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 

 

Hakimu Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo, aliwaeleza washtakiwa hao kuwa dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili. Hata hivyo, walishindwa kutimiza masharti na kupelekwa mahabusu. 

 

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 9 mwaka huu.

Awali, akiwasomea mashtaka, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo Aprili 19, mwaka huu, jijini Dar es Salaam kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Namba 7 ya mwaka 2011. 



Katika shtaka la kwanza, Wakili Lekayo alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja na wengine ambao hawajakamatwa, waliomba rushwa Sh50 milioni kutoka kwa Clarke. 

 

Wakili Lekayo, alidai katika shtaka la pili washtakiwa hao kwa pamoja na wengine ambao hawajakamatwa bado, walijihusisha na vitendo vya kumuomba rushwa ya Sh5 milioni mkurugenzi huyo ili wampunguzie kodi kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni. 

 

Katika Shtaka la tatu, Wakili Lekayo alidai washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kupokea rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa Clarke ili wampunguzie kodi kutoka Sh375 milioni mpaka Sh100 milioni.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment