Serikali
imepanga mwaka ujao wa fedha kununua magari mengi kwa ajili ya
kuyasambaza kwenye vituo tofauti vya Polisi nchini vyenye uhaba.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema mpango huo utatekelezwa katika bajeti ya mwaka 2016/17.
Alisema
hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Musa Ntimizi (CCM),
aliyehoji kama wizara haioni umuhimu wa kuvipatia magari vituo vya
polisi ambavyo havina magari katika jimbo hilo ili kurahisisha utendaji
kazi.
Mbunge
huyo pia alitaka wizara kumalizia ujenzi wa kituo cha polisi kikubwa
kilichojengwa katika kata ya Loya halmashauri ya Tabora (Uyui) ambapo
kwa sasa wananchi wameishiwa nguvu ya kuendeleza ujenzi huo.
Waziri
alisema, serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na wananchi katika
kuchangia maendeleo, alimtaka mbunge huyo kuwasiliana na wizara yake ili
waweze kuona namna ya kusaidia kumalizia ujenzi wa kituo hicho ili
kianze kufanya kazi.
Katika
swali la msingi, mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini kituo cha Loya
kitafunguliwa hasa ikizingatiwa kuwa Loya ni zaidi ya kilomita 120
kutoka makao makuu ya Wilaya Isikizye ambapo ndiko kwenye kituo cha
polisi.
Pia
alihoji serikali ina mpango gani wa kuwaongezea bajeti ya mafuta
kuwarahisishia watendaji kazi, maana maeneo ya jimbo ni makubwa na yote
yanahitaji huduma za kipolisi.
Akijibu
swali hilo, Kitwanga alisema pamoja na mwitikio wa wananchi na wadau
kujenga kituo hicho, bado hakijakamilika sehemu ya kuhifadhi silaha,
huduma ya choo na makazi ya askari.
Waziri huyo alisema, pindi hivyo vitu vitakapokamilika kituo hicho kitafunguliwa na askari watapelekwa.
Alisema,
serikali ina mpango wa kuongeza bajeti ya mafuta katika maeneo
mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha, ili kukidhi mahitaji ya
doria, misako na operesheni mbalimbali katika kutoa huduma ya ulinzi na
usalama kwa wananchi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment