WIZARA
ya Maliasili na Utalii imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi la Taifa
(TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa
jeshi usu (Paramilitary) ili kukabiliana na tatizo sugu la ujangili wa
wanyamapori, misitu, na rasilimali nyingine za nchi.
Akizungumza
wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi wa shirika hilo, Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya
shirika hilo kutaka kubadilishwa na kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni
ya msingi katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na tatizo
sugu la ujangili wa wanyamapori.
Ufungaji
wa mafunzo hayo ulifanyika juzi katika kambi ya Mlele ndani ya Hifadhi
ya Taifa ya Katavi mkoani Katavi ambako askari 101 na wahifadhi 26
walihitimu mafunzo ya kijeshi ya miezi mitatu hadi sita
“Kwa
sasa uhifadhi unakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili,hususan tembo
na faru kuporomoka kwa maadili ya askari na uingizaji wa mifugo
hifadhini,” alisema Meja Jenerali Milanzi.
Aliongeza: “Maombi
yenu yamekuja kwa wakati muafaka hivyo tutawasilisha katika mamlaka
nyingine za juu za kiserikali, ili yatungiwe sheria na hatimaye
kuwasilishwa bungeni ili yajadiliwe na kupitishwa kuwa sheria.”
Hata
hivyo, aliwataka askari hao pamoja na Menejimenti ya Tanapa kufanya
maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa baadhi ya
mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kama
ilivyo kwa majeshi mengine nchini.
Awali
akiwasilisha maombi hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi
alisema shirika hilo baada ya kutafakari kwa kina wakitumia wataalamu wa
ndani ya shirika walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za
kijeshi kutokana na changamoto ya sasa ya katika masuala ya uhifadhi.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga alielezea
umuhimu wa kutunza maeneo yaliyohifadhiwa huku akionya kuwa makundi ya
wafugaji yanayovamia maeneo hayo lazima yaondolewe haraka.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment