WAKATI mashabiki wakitabiri kiwango cha kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Juma Mahadhi kuwa kitamuweka benchi Simon Msuva, mwenyewe ameibuka na kudai yeye anamuomba Mungu asipatwe na majeraha na kitakachofuata wao wenyewe watakubali mziki wake.
Mahadhi aliyesajiliwa na Yanga hivi karibuni akitokea Coastal Union, Jumanne ya wiki hii alizua gumzo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha katika mchezo dhidi ya TP Mazembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ikiwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilikuwa hivi, Msuva alipata ugonjwa wa malaria muda mfupi kabla ya mchezo huo, ikabidi Kocha Hans van Der Pluijm amtaje Mahadhi kuwa ataanza katika kikosi cha kwanza, wengi walipata mshtuko kwa kuwa ilikuwa mechi yake ya kwanza kubwa kuanza kuichezea Yanga akiwa hana uzoefu hata kidogo.
Kilichotokea baada ya hapo ni kuwa Mahadhi alionyesha kuwa anaweza ambapo alifanya mambo makubwa licha ya Yanga kupoteza mchezo huo, hali ambayo ikasababisha wengi wajiulize juu ya hatima ya Msuva.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Msuva alisema anampongeza Mahadhi kwa kiwango kikubwa alichokionyesha akicheza mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na Yanga kwa kufanikiwa kuendana na kasi ya timu.
“Mimi kila siku ninamuomba Mungu nisipatwe na majeraha na siyo kitu kingine, kwa sababu kama nikipata majeraha ni lazima nikae nje na mchezaji mwingine kuchukua nafasi yangu,” alisema Msuva na kuongeza:
“Hata simdharau Mahadhi kwani ni mchezaji mzuri na ninaheshimu uwezo wake ndani ya uwanja, ninafikiri kila mtu alimuona katika mechi na Mazembe, lakini kwangu hatapata nafasi ya kucheza labda nipate majeraha makali yatakayonifanya nishindwe kucheza.
“Ninafurahia changamoto yake ya ndani ya uwanja inayonifanya nisibweteke zaidi niongeze bidii na kujituma kwenye mazoezi yangu binafsi na timu.”
Mara baada ya mchezo huo wa Jumanne, mashabiki na wanachama wa Yanga wengi walionekana kumsifia Mahadhi na kusema Yanga imepata mchezaji mwenye kiwango kizuri na anayeweza kuwa na faida kubwa kama ataendelea kucheza kwa kiwango cha juu katika nafasi ya kiungo mshambuliaji wa pembeni.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment