Basi la JM Luxury Lapata Ajali na Kuua Watu Wanne Mwanza

WATU wanne wamekufa huku sita wakijeruhiwa katika ajali ya basi, lililogonga lori katika eneo la njiapanda ya Kolandoto mkoani Mwanza.
Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya JM Luxury kuligonga lori aina TATA, lenye namba za usajiri T218 ABY, la Kampuni ya Birichand lililokuwa likitoka mjini Shinyanga kwenda Kishapu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Elias Mwita alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo saa 11 .15 alifajiri jana.
Alieleza kuwa ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi wa basi hilo lililokuwa likitoka Shinyanga kwenda Mwanza.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, watu wanne waliokufa walikuwa ndani ya lori, ambalo liligongwa na basi upande wa kulia.

Alisema mbali na kuwa katika mwendo kasi, basi hilo lilitaka kulipita lori hilo ambalo lilikuwa linaanza kukata kona kuelekea wilayani Kishapu, hivyo kuligonga kwenye kichwa na kusababisha vifo hivyo.

Kamanda Mwita hakutaja waliokufa katika ajali hiyo, lakini alisema miili yao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.

Majeruhi wamelazwa hospitali hiyo na Hospitali ya Kolandoto. Alitaja majeruhi wanne waliolazwa katika Hospitali ya Kolandoto kuwa ni Salehe Kassim (46) ambaye ni dereva wa basi na Mohamed Ahmed (39) ambaye ni kondakta wa basi.

Abiria waliolazwa ni Valencia Magingi (34) aliyepo Hospitali hiyo ya Kolandoto na waliolazwa Hospitali ya Mkoa ni Joseph Mkunda (58) na Salome Paulo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dk George Herberth alikiri kupokea majeruhi wawili ambao ni Salome Paulo aliyepata majeraha na kuvunjika mguu wa kulia ambaye anaendelea na matibabu huku Joseph Mkunda akipata matibabu na kuruhusiwa kuondoka. Miili ya waliokufa imehifadhiwa hospitalini hapo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment