Majengo ya Bunge Yachomwa Moto Kisa Ali Bongo Kutangazwa Rais,

Fujo zimezuka katika Mji Mkuu wa Gabon, Libreville baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa jana Jumatano mchana kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi iliyopita, Agosti 27, 2016, kwa kupata asilimia 49.8% ya kura, akifuatwa na mpinzani wake Bw Ping aliyepata asilimia 48.2 % ya kura, huku wa kitofautiana kura 5,594 pekee.
Jean Ping
Mgombea wa upinzani kwenye uchaguzi huo, Jean Ping ambaye pia ni shemeji wa rais Ali Bongo amesema watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya vikosi vya usalama kuvamia makao makuu ya chama chake.
Serikali imesema inawaandama “wahalifu wenye silaha” ambao awali walikuwa wameteketeza majengo ya bunge.
Bw Ping amepinga matokeo ya urais ambayo yalionyesha Rais Bongo alishinda uchaguzi kwa kura chache. Hii inampa fursa ya kuongoza taifa hilo kwa muhula mwingine wa miaka saba.
“Walishambulia mwendo wa saa 01:00 (00:00 GMT). Ni kikosi cha wanajeshi walinzi wa rais. Walikuwa wanarusha mabomu kutoka kwa helikopta na kisha baadaye wakashambulia kutoka ardhini,” Bw Ping, ambaye hakuwa katika makao makuu hayo wakati huo, alisema awali.
Rais Ali Bongo
Ping ameomba usaidizi kutoka kwa jamii ya kimataifa kulinda raia huku akieleza kuwa uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na “hakuna ajuaye” hasa nani alishinda.
Waandamanaji waliingia barabarani muda mfupi baada ya tangazo kutolewa na kuchoma moto majengo ya bunge na kukabiliana na polisi wa kuzima fujo.
Upande wa Bw Ping unasema takwimu kutoka ngome za rais huyo zinaonesha asilimia 99 ya wapiga kura walijitokeza. Ameomba takwimu za wapiga kura kutoka kila kituo zitolewe wazi.
Marekani na Umoja wa Ulaya wametoa wito kura hizo ziwekwe wazi huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon naye akihimiza utulivu.
Bw Bongo aliingia madarakani mwaka 2009, baada ya kifo cha babake aliyechukua madaraka 1967.
Kabla ya kuingia kwenye siasa, Bw Ping alikuwa mwanadiplomasia ambaye alihudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment