Tume Ya Mufti Yawaita Wanaojua Wezi Bakwata

TUME iliyoundwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi kuchunguza mali za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), imeomba watu wenye taarifu juu ya ubadhirifu wa mali za taasisi hiyo wawasiliane nao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Sheikh Issa Othman Issa aliomba pia ushirikiano wa watu wenye taarifa juu ya mali za baraza hilo.

Sheikh Issa aliahidi kuwa tume yake itawalinda wale wote watakaowapa taarifa zozote zitakazosaidia katika uchunguzi wao.

“Tunaendelea kuwaomba wale wenye taarifa za mali za Waislamu ambazo ziko chini ya usimamizi wa Bakwata wawasiliane na tume ikiwamo kukabidhi nyaraka zote walizonazo, hata wenye ushahidi wowote wa ubadhirifu wa mali wazilete tunaahidi kwa dhati tutazifanyia kazi na kuwalinda watoa taarifa, tume hii ni huru ina ruhusa ya kuendesha kazi zake bila kuingiliwa na mtu ama chombo chochote,” alisema Sheikh Issa.

Alisema katika kufanikisha kazi hiyo waliyopewa, tume hiyo inafanya kazi na jopo la wataalamu na vyombo mbalimbali vilivyobobea katika masuala hayo.

Sheikh Issa alisema wamepewa hadidu za rejea saba ikiwamo kuchunguza misamaha ya kodi iliyotolewa kwa baraza na taasisi zake.

Kuundwa kwa tume hiyo ni matokeo ya ushauri uliotolewa na Rais John Magufuli, Julai mwaka huu alipokuwa akihutubia Baraza la Eid ambapo pia aliahidi kuzirejesha mali zilizoporwa za waumini wa dini hiyo.

Sheikh Issa alisema kuwa wamepewa miezi mitatu kukamilisha uchunguzi huo.

Alitaja mambo watakayochunguza kuwa ni pamoja na misamaha ya kodi iliyoombwa na Bakwata nchi nzima, mikataba yote ya uuzaji wa viwanja na mali mbalimbali za baraza na taasisi zake pamoja na uhalali wa umiliki wake.

Nyingine ni kutafuta mikataba yote ambayo baraza na taasisi zake zimeingia na wawekezaji na kuona mikataba hiyo kama ina maslahi na baraza au laa, na kuchunguza mikataba yote ambayo taasisi zake nchi nzima zimeingia na wapangaji wake katika maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na baraza hilo.

Nyingine ni kuchunguza mali zote za baraza na kuona hali ya usajili wa mali hizo na kuchunguza mapato na matumizi ya baraza hilo na taasisi zake nchi nzima.

Sheikh Issa alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika ndani ya siku hizo 90 watakabidhi ripoti hiyo kwa Mufti kwa ajili ya hatua nyingine zaidi.

Wakati huo huo, swala ya Eid El-Hajj inatarajiwa kuswaliwa leo makao makuu ya Bakwata, yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Katibu wa Baraza hilo, Salim Abeid, swala hiyo itaambatana na Baraza la EID na kufuatiwa na uzinduzi wa Chuo cha Kiislam.
Abeid alisema swala hiyo itafanyika saa moja na nusu asubuhi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment