VIFAA
vilivyokamatwa jana vya klabu ya usiku ya Bilicanas na ofisi ya gazeti
la Tanzania Daima, vyote vinavyomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, vitapigwa mnada na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) siku 14 kuanzia jana, endapo atashindwa
kulipa Sh. bilioni 1.2 za deni la pango la miaka 20.
Mbowe
alikuwa mpangaji katika jengo la NHC lililopo makutano ya mitaa ya
Mkwepu na Indira Gandhi, katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Vyombo
hivyo vilikamatwa jana na kampuni ya udalali ya Fosters Auctioneers and
General Traders iliyopewa kazi ya kuondoa vifaa hivyo baada ya Mbowe
kushindwa kulipa deni hilo ndani ya miezi miwili ya notisi ambayo
shirika hilo lilikuwa limempatia.
Meneja
wa Kitengo cha Kukusanya Madeni kutoka NHC, Japhet Mwanasenga aliyekuwa
akisimamia ukamataji wa vyombo hivyo, alisema Mbowe ana muda wa wiki
mbili kuanzia jana kulipa deni la Sh. bilioni 1.172 vinginevyo vitapigwa
mnada.
Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na kompyuta, meza na viti.
Alisema
taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumuondoa mteja wao, ikiwamo notisi
na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo wa wiki mbili.
“Tunashikilia
vyombo kwa muda wa wiki mbili na iwapo atashindwa kulipa vitapigwa
mnada na dalali, (mdaiwa) akishindwa kulipa anapangishwa mwingine,” alisema.
Alisema
shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa
majengo yake hivyo mteja ambaye anadaiwa ajiandae kuondolewa wakati
wowote na kwamba zoezi la jana ni mwanzo tu.
Baadhi ya watu wamelihusisha tukio la kuondolewa Mbowe katika ofisi hizo na masuala ya kisiasa.
Lakini Mwanasenga alisema uamuzi wa kumuondoa ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya kisiasa.
Alisema
wapangaji wa jengo hilo wapo wengi pamoja na wadaiwa na kwamba baada ya
mchakato huo kuanza mdaiwa yeyote atakayeshindwa kulipa kodi
ataondolewa.
Akizungumza
na waandishi wa habari katikati ya wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa
NHC, Nehemia Mchechu alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai
taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.
Notisi
ya siku 60 ya kuondoka Bilicanaa pamoja na majengo ya wadaiwa wengine
ilishatolewa, Mchechu alisema. Notisi hiyo ilikuwa inaisha juzi.
Alisema
baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo
hayo utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za kisheria.
Mchechu
alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni
161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadiawa
wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni
mbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.
Mchechu
alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo
kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia
Dodoma.
"Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema Mchechu, hivyo "fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini humo."
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.
Alisema
shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino,
nne Bahi na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono azma ya serikali
ya awamu ya tano kuhamia Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment