Askofu Awataka Mafisadi na Wahujumu Uchumi Wajitumbue MAJIPU Wenyewe

Wahujumu uchumi, mafisadi na wote wanaokiuka viapo vyao wametakiwa kujitumbua majipu wenyewe badala ya kusubiri Rais John Magufuli, kwa kuungama kwa viongozi wao wa dini ili kusafisha nafsi zao.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Paroko wa Kanisa Katoliki mjini Mugumu wilayani Serengeti, Alois Magabe wakati wa ibada ya mkesha wa Pasaka.

“Hawa watu wanapaswa kumpata Mungu kwa kuungama kwa sababu matendo yao siyo tu dhambi, bali yana madhara na udhalimu kwa umma kijamii, kiuchumi na hata kisiasa,” alisema Padri Magabe na kuongeza:

“Matendo ya uhujumu uchumi, ufisadi, wizi na ushirikina yanawatenga wanadamu na Mungu, wahusika lazima watubu na kurejea katika njia safi badala ya kusubiri kutumbuliwa na Rais,” alisema Padri Magabe.

Aliwataka waumini wa dini na madhehebu yote kutumia maadhimisho ya sikukuu za kidini kuhimiza matendo mema, kutimiza wajibu, haki, heshima kwa utu wa mwanadamu na usawa kwa wote bila kujali tofauti miongoni mwao.

Naye Askofu Naamon Kajeri wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMKT) Jimbo la Mara, aliwataka viongozi wa Serikali na siasa ngazi zote kuongoza kwa hofu ya Mungu, kutimiza kwa vitendo maandiko kuwa mamlaka zote duniani zinawekwa na Mungu.

Askofu Kajeri aliwata wote wenye dhamana kutenda haki na kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka misingi, ili dhana ya usawa isimame na kuonekana miongoni mwa wananchi. 
Alisema kuendelea kuhubiri dhana hiyo bila kuisimamisha, haina maana yoyote.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment