Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema mkoa wake hauko
salama kama watu wanavyodhani kwa sababu silaha nyingi zinamilikiwa
kiholela na mafunzo ya matumizi ya silaha hizo hutolewa hata kwa watoto.
Makonda alisema hayo jana wakati wa ibada ya Pasaka
iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano na kuwataka
wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kuhakiki silaha zao na kusalimisha
zile zinazomilikiwa kinyume cha sheria.
Alisisitiza kwamba
ifikapo Julai Mosi, operesheni maalumu ya kukamata silaha zinazomilikiwa
kinyume cha sheria itaanza na yeye mwenyewe ndiye atakayeiongoza.
“Tumegundua
kwamba kwenye bonde la mto unaotenganisha Mkoa wa Dar es Salaam na
Pwani, kuna mafunzo yanatolewa kwa watoto. Wazazi wanadhani watoto wao
wamekwenda shule kumbe wamechukuliwa huko.Hatuwezi kukubali hali hiyo iendelee."Alisema
Mkuu
huyo wa mkoa aliwataka waumini waendelee kumuombea ili afanye kazi yake
vizuri kwa kutenda haki pia aliwataka pia wamwombee Rais Magufuli kwa
sababu kazi anayoifanya ni kubwa.
Alisema
Rais anapotumbua jipu moja,ndani yake kuna kundi la watu wanaoathirika
na hatua aliyoichukua hivyo, alisema watu wa aina hiyo hawawezi
kumpenda kwa sababu amevunja mtandao wa masilahi yao.
“Ninaomba
kanisa pamoja na viongozi wote wa dini mnisaidie katika kuhimiza suala
la ulinzi na usalama ili amani yetu iendelee kudumu. Ninaomba
tushirikiane katika hilo, Dar es Salaam haiko salama kama mnavyodhani,
mengine siwezi kusema kwa sababu sijaruhusiwa na Rais,” alisema.
Migogoro kanisani
Akizungumzia migogoro makanisani, Makonda alisema
hataki kusikia kiongozi yeyote wa dini anakimbilia polisi au mahakamani
kutaka suluhisho la matatizo yao ya ndani na kuwa atamweka ndani
atakayejaribu kufanya hivyo.
Alisema ni aibu kubwa kwa kanisa
kukimbilia kwenye vyombo vya dola badala ya polisi na Serikali
kukimbilia kanisani kuomba ushauri. Alisema kanisa ndicho chombo cha
usuluhishi wa matatizo mbalimbali ya jamii.
“Serikali inahitaji
msaada wa kanisa na viongozi wa dini ili iweze kufanya kazi vizuri.
Sitaki kusikia polisi wanakwenda kanisani (kukamata watu) katika mkoa
wangu na wale wanaotoa taarifa kutaka polisi nitawaweka ndani,” alisema
Makonda ambaye kabla ya kuwa mkuu wa mkoa, alikuwa mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni.
Askofu Mokiwa
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana,
Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa alibainisha mambo mbalimbali
aliyoyaita majipu ambayo yanafanya kanisa hilo lisiendelee katika
kufundisha waumini wake yaliyo mema.
Mokiwa alitaja mambo hayo
kuwa ni pamoja na mashindano ya kimadhehebu. Alisema madhehebu
mbalimbali yanashindanishwa kupima kanisa lipi ni kubwa, lina waumini
wangapi, linamilikiwa na nani na nguvu yake ni ipi.
Jambo
jingine alisema ni maaskofu wenyewe kupigana vita. Alisema sasa ni
kawaida kwa askofu mmoja kumchimba mwingine, askofu mmoja kupanga
mapinduzi dhidi ya mwingine na baadhi ya maaskofu kutukanana waziwazi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment