KAPOMBE Ajazwa Mapesa ya Uchezaji Bora wa Ligi ya Vodacom

Kapombe2 Beki wa Azam FC, Shomari Kapombe (kushoto) akiwa ameshikilia hundi yenye thamani ya Sh. Milioni 1/- kama tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) jana katika mazoezi ya timu yake, Kutoka kulia ni Ofisa wa Bodi ya Ligi (TPLB), Joel Balisidya, Ofisa Matukio na Udhamini wa Vodacom, Ibrahim Kaude pamoja na Meneja wa kikosi hicho, Luckson Kakolaki.
Mchezaji wa timu ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam Shomary Kapombe jana amekabidhiwa kitita cha shilingi Milioni 1/- kutokana na kuibuka kuwa mchezaji bora wa ligi ya soka ya VPL inayoendelea kwa kipindi cha mwezi Januari mwaka huu.

Kapombe amekabidhiwa kitita hicho kutoka kwa mdhamini wa waligi hiyo Vodacom Tanzania katika uwanja wa klabu anayoichezea uliopo maeneo ya Chamanzi,jijini Dar es Salaam.

Akiongea muda mfupi baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo ikiwa ni tuzo ya uchezaji bora,Kapombe alisema amefurahia kuwa miongoni mwa wachezaji waliopata tuzo tuzo na kuongeza kuwa imezidi kumtia moyo na bidii ya kujituma zaidi.

“Nashukuru Vodacom kwa kuwapatia zawadi wachezaji wanaofanya vizuri kwa kuwa inawazidishia kasi ya kujituma zaidi,pia nawashukuru wachezaji wenzangu wote wa Azam maana bila jitihada za pamoja sio rahisi mchezaji mmoja ukaibuka na kuonekana bora kwa kuwa katika mchezo wa soka sote tunategemeana”. Alisema.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania,Matina Nkurlu aliyeambatana na Ofisa wa Bodi ya Ligi, Joel Balisidya pamoja na Ofisa Udhamini na Matukio wa kampuni hiyo, Ibrahim Kaude katika kumkabidhi zawadi hiyo alimpongeza mchezaji huyo na kuongeza kusema kuwa Vodacom inajivunia mafanikio yanayoendelea kupatikana katika ligi hiyo na ina mpango wa kushirikiana na wadau wengine wa soka kuzidi kuiboresha zaidi.

Kapombe alitwaa tuzo mwezi Januari uliokuwa na raundi tatu, alicheza dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na Mgambo Shooting.

Mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa kiporo, na ilichezwa Februari 24, 2016.

Kapombe alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia alisaidia kupatikana bao la Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande wake.

Washindani wa Kapombe kwenye kinyang’anyiro hicho katika mwezi huo walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment