Panya Road, Majambazi Wanaovaa Madera Jijini Dar Kusakwa Nyumba Hadi Nyumba!

IMG_1908 Kamanda Muroto.
Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke jijini Dar, ACP Gilles Muroto amesema wahalifu wote, wakiwemo Panya Road na majambazi wanaovaa mavazi aina ya madera wakati wakifanya uhalifu, watasakwa nyumba hadi nyumba hadi watokomezwe.
Tamko hilo kali alilitoa wiki iliyopita katika mkutano wake na wananchi uliofanyika Mtaa wa Machinjioni, Kata ya Mianzini, Temeke ambapo aliwataka wahalifu wote kujisalimisha na kutafuta kazi halali, vinginevyo watakaokaidi watakiona cha moto.
Kamanda huyo amekuwa akifanya mikutano kwa kila kata inayojumuisha mitaa yote ili kuwahamasisha wananchi kushirikiana na polisi kukomesha uhalifu na kuwataka viongozi wa serikali ya mitaa kuanzisha vikundi vya vijana vya ulinzi shirikishi.
IMG_1914Kamanda Muroto akiongea na wananchi.
Aidha, kamanda huyo aliwataka wazazi kuacha mara moja tabia ya kuwatoa watoto wao shule na kuwapa mafunzo ya kiuhalifu ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutumia bunduki. Alitoa kauli hiyo kufuatia operesheni kali iliyofanyika katika msitu wa Mkuranga, Mkoa wa Pwani ambapo watu zaidi ya 120 wakiwemo watoto wa chini ya umri wa miaka sita walioachishwa masomo walikamatwa.

“Wananchi toeni taarifa juu ya vijana wanaovuta bangi katika maeneo yenu, au ya shule ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo ya sheria.

“Tuendelee kudumisha amani iliyopo kwani nchi nyingi zinazotuzunguka zenye migogoro watu wake wamekuwa wakikimbilia hapa kutokana na utulivu, je hali hiyo ikitoka hapa kwetu tutakimbilia wapi? Nimewataka wale wote wanaocheza pool na kunywa pombe wakati wa kazi, wanaokaa katika vijiwe vya video waache mara moja, nimewaamuru polisi kuwakamata,”alisema Kamanda Muroto.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment