Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Laridhishwa na Serikali ya MAGUFULI Katika Mapambano ya Rushwa

Ujumbe wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) umeridhishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli katika kuongeza juhudi za kupambana na rushwa. 
Hali hiyo itabadili mtazamo wa awali kwamba utawala bora ulishapotea nchini, kama ilivyoonekana katika tafiti nyingi zilizofanyika.

Aidha, ujumbe huo unaunga mkono malengo ya uchumi yaliyomo katika mwongozo wa Bajeti ya mwaka 2016/2017 uliochapishwa, ambayo yamezingatia uhalisia katika ukadiriaji wa mapato.

Hayo yalielezwa katika taarifa ya shirika hilo, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa ziara ya ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi Msaidizi na Mkuu wa IMF nchini, Herve Joly.
 Ujumbe huo pia ulifanya tathmini ya nne ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi (PSI), ulioidhinishwa na Bodi Tendaji ya IMF mwaka huu.

Ilieleza taarifa hiyo kuwa “ujumbe umeridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali katika kuongeza juhudi zaidi za kupambana na rushwa, hali ambayo itabadili mtizamo wa awali kwamba utawala bora ulikwishapotea nchini kama ilivyoonekana kwenye tafiti nyingi zilizofanyika.”

Tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana, Rais John Magufuli na serikali yake imejipambanua kwa kupambana na rushwa na ufisadi kwa kuwachukulia hatua wakwepa kodi na watendaji wa serikali ambao ni wala rushwa, kuwapeleka mahakamani na kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwongozo wa bajeti ya Tanzania kwa mwaka 2016/17 umezingatia kupunguza kwa kiasi kikubwa nakisi ya bajeti na matumizi ya kawaida ili kutoa fursa ya kuongeza matumizi ya maendeleo.
“Changamoto kubwa katika kukamilisha bajeti ni kuhakikisha kuwa matumizi yanaendana na mapato halisi. Majadiliano yataendelea katika wiki chache zijazo ili kufikia muafaka juu ya mfumo mzima wa sera za uchumi ambazo zitapelekwa kukamilisha mapitio ya nne ya mpango wa PSI,” ilieleza taarifa hiyo.

Mapitio hayo ya mpango wa PSI na majadiliano chini ya kanuni ya nne ya mkataba ulioanzisha IMF, yanatarajiwa kujadiliwa na Bodi Tendaji ya IMF mwaka huu. 
Majadiliano chini ya mpango wa PSI pia yamelenga kwenye utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 na mipango ya bajeti ya mwaka 2016/2017.

Katika taarifa hiyo, Joly alisema mwenendo wa uchumi umeendelea kuimarika kwani makadirio yanaonesha kuwa Pato la Taifa kwa mwaka jana lilikua kwa asilimia saba, huku shughuli zilizokua kwa kasi ni ujenzi, mawasiliano, huduma za kifedha na uchukuzi. 
“Mfumuko wa bei umeendelea kubakia kwenye kiwango cha tarakimu moja muda wote wa mwaka 2015 na kufikia wastani wa asilimia 5.6, japokuwa thamani ya Shilingi ilishuka kwa kiasi kikubwa katika nusu ya mwaka,” alisema Joly.

Alisema majadiliano na serikali chini ya kanuni ya nne ya mkataba wa IMF yalijikita kwenye namna ya kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa kiwango cha juu unaozingatia utekelezaji wa vipaumbele vya serikali bila kusababisha athari za kiuchumi. 
Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya kimfumo yanahitajika ili kuboresha mfumo mzima wa kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji na uwekezaji.

“Kumekuwa na mtazamo sawa wa maoni kwenye maeneo ya vipaumbele vya maboresho ya kiuchumi na jinsi serikali itakavyochangia katika kuwezesha uchumi endelevu na unaoongozwa na sekta binafsi,” aliongeza Joly.
 Alisema uboreshaji wa sekta ya kilimo inayoajiri idadi kubwa ya watu utasaidia kuongeza kipato cha watu wa vijijini na hiyo kuchangia kupunguza umasikini.

Aidha, utatoa fursa ya ajira kwa sekta nyingine za uchumi na kukuza viwanda mbalimbali ikiwemo vya kusindika vyakula. Kipaumbele kingine ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa nishati na miundombinu bora ya usafirishaji na upatikanaji wa ardhi na mitaji.

Aidha, kuendelea kuimarisha hali ya kifedha ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kulipa malimbikizo ya madeni ya huduma za gesi na umeme ni muhimu katika kuwawezesha wawekezaji binafsi kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya nishati. 
“Tanzania inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na kukamilika kwa soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo litasaidia kuvutia mitaji na kukuza ushinda na kuongeza ufanisi,” alisema.

Wakati huo huo, mapato ya serikali kwa mwezi huu yamefikia Sh trilioni 1.4, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Mpango alieleza mchanganuo wa fedha hizo kuwa ni mapato ya kodi (Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA) ni Sh 1,283,274,000,000, mapato yasiyo ya kodi Sh 77,504,000,000 na mapato yatokanayo na vyanzo vya Halmashauri Sh 43,490,000,000, kufanya jumla ya Sh 1,404,268,000,000.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment