Lahore, Pakistan
KUNDI moja lililojitenga kutoka kwa
wapiganaji wa Taliban limesema ndilo lililotekeleza shambulio la kujitoa
mhanga mjini Lahore, Pakistan lililoua watu zaidi ya 70 na takriban
watu 300 wakijeruhiwa jana Jumapili.
Kundi hilo la Jamaat-ul-Ahrar lilisema
liliwalenga Wakristo waliokuwa wakisherehekea Pasaka, ingawa polisi
wamesema bado wanachunguza madai hayo huku wakiongeza kuwa huenda idadi
ya waliokufa ikaongezeka zaidi.
Lahore
ni mji tajiri na ni mojawapo wa miji yenye mtazamo huru zaidi nchini
Pakistan. Pia ndiyo ngome ya kisiasa ya Waziri Mkuu wa sasa wa nchi
hiyo, Nawaz Sharif, na haujawahi kushambuliwa kigaidi kwa miaka ya
karibuni.
Mlipuko huo ulitokea kwenye bustani ya
Gulshan-e-Iqbal mjini Lahore karibu na eneo la kuchezea watoto Jumapili
jioni. Kulikuwa na hali ya kutamausha wazazi wakiwatafuta watoto wao
kwenye vifusi.
Rais wa Pakistan ameshutumu shambulio hilo na serikali ya jimbo imetangaza siku tatu za maombolezo.
Msemaji wa kundi la Jamaat-ul-Ahrar,
Ehsanullah Ehsan, alisema kundi hilo lilitaka kutuma ujumbe kwa Bw.
Sharif kwamba wameingia Lahore na akasema kundi hilo litatekeleza
mashambulio zaidi.
Jamaat-ul-Ahrar walijitenga kutoka kwa
Tehrik-e Taliban Pakistan. Limetekeleza mashambulio mengine kadha dhidi
ya raia na vikosi vya usalama miezi ya hivi majuzi.
Bw Sharif ameeleza masikitiko yake na
huzuni kutokana na watu wengi wasio na hatia waliopoteza maisha yao.
Ameahirisha ziara aliyokuwa amepanga kuifanya nchini Uingereza.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment