AMUUA MWENZAKE KISA POMBE ZA VIROBA

POLISI mkoani Katavi inamshikilia Pisikitu Michael (39) kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea pombe za viroba, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema.Michael anatuhumiwa kumpiga Shukuru Korongo (32) na kumsababishia maumivu na baadaye marehemu huyo kufariki dunia, wakati wakigombea viroba kwenye sherehe ya jirani yao.

Kaimu Kamanda Nyanda alisema mauaji hayo ni matokeo ya kupigana kulikoanza baada ya mmoja wao kufyonza kwa haraka viroba vyake na kutaka kuchukua vya mwenzake.
Alisema tukio hilo lilitokea Jumatano saa 5.00 usiku wakati wakiwa kwenye sherehe ya mtoto mchanga aliyekuwa anatimiza siku 40 tangu kuzaliwa.


Alisema wakiwa wanafurahia viroba hivyo, Michael aliwahi kumaliza vyake na kumuomba rafiki yake amgawie kwa kuwa Korongo alikuwa anakunywa polepole.
Hata hivyo mwenzake huyo alikataa, alisema Nyanda.
Baada ya kukataliwa, alimnyang’anya huku Korongo akikataa kumpa akieleza kuwa wote walipewa viroba vinne kila mmoja.


Marehemu alimtaka Michael aondoke akalale, kama amemaliza viroba vyake “na awaachie wenye pombe zao waendelee na sherehe.”
Kaimu Kamanda alisema baada ya kuvutana walianza kupigana hadi ikiwalazimu watu kuingilia kati na kuwaamulia.


Baada ya muda mfupi Korongo alianza kulalamika anasikia maumivu makali tumboni, alisema Nyanda, hali iliyosababisha arudi nyumbani kulala na kuacha watu wakiendelea na sherehe hizo usiku huo.
Ilipofika asubuhi, Kaimu Kamanda alisema, mama yake Korongo alikwenda kumuona mwanae lakini alipogonga mlango huku akimwita hakupata jibu kutoka ndani.


Mama huyo aliamua kuusukuma mlango kwa nguvu na ulipofunguka aliingia ndani na kukuta mtoto wake amekwishafariki dunia akiwa kitandani hapo, alisema Kaimu Kamanda huyo.
Mama huyo alikwenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo kutoa taarifa, na baada ya kuzipokea Mwenyekiti huyo Margaret Kitunguru alikwenda polisi kuripoti, alisema Nyanda.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Katavi Nyanda alisema mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi wakati upelelezi ukiendelea.
CREDIT – NIPASHE
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment