BENKI YA DUNIA KUIPA TANZANIA DOLA MILIONI 65

BENKI ya Dunia imepanga kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kuboresha utendaji wa Idara ya Mahakama kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kusogeza haki jirani zaidi na wananchi.
 
Rais wa Benki ya Dunia Jim Young Kim

Hatua hiyo ilifikiwa jijini Washington, Marekani jana baada ya Bodi ya Juu ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia kupitia taasisi yake inayoshughulikia utoaji wa misaada na mikopo nafuu kwa mataifa masikini duniani (IDA) kuidhinisha mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 65 kwa Tanzania ili kuweza kusaidia Mpango wa Maboresho ya Mhimili wa Mahakama ili kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa kupata huduma za Mahakama.
Mradi huo mpya umeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa na pia katika Mpango Mkakati wa Maboresho ya Idara ya Mahakama wa mwaka 2015-2025.

Kupitia mipango hiyo, Serikali imelenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza uwazi, uwajibikaji na kupunguza umasikini.
Mpango wa Maboresho katika Mhimili wa Mahakama utaongeza ufanisi katika utekelezaji wa vipaumbele vya taifa kwa kusaidia kuboresha utoaji wa huduma na pia kuongeza wigo wa upatikanaji wa haki.

“Kuna idadi kubwa sana ya Watanzania ambao kwao upatikanaji wa huduma za kimahakama ni mgumu kutokana na ugumu wa gharama, lakini haipaswi kuwa hivyo kwa vile ni suala muhimu kwa ustawi wa maisha ya jamii na maendeleo ya watu wake,” alisema Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia katika mataifa ya Tanzania, Burundi, Somalia na Malawi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment