Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein
amesema dhamira ya Serikali ni kuona watumishi wake wanapata maslahi
mazuri zaidi ili kumudu gharama za maisha.
Pamoja
na dhamira hiyo, hata hivyo, utekelezaji wake utategemea zaidi ukuaji
wa uchumi ambao utatoa mapato zaidi kwa ajili ya kugharimia uendeshaji
wa shughuli za serikali ikiwemo mishahara, alisema Dk. Shein.
Akizungumza
na ujumbe wa viongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi
Zanzibar (ZATUC) ofisini kwake Ikulu jana, Dk. Shein alisema viongozi wa
wafanyakazi wanapaswa kuelewa hali halisi ya mapato ya serikali na
ugumu unaoambatana na kuongeza maslahi ya watumishi bila kuzingatia
mapato halisi ya serikali.
“Sisi
(serikali) wafanyakazi wametuchagua kuwaongoza na nyinyi (viongozi wa
ZATUC) ni hivyo hivyo wamewachagua kuwawakilisha. Kwa hivyo ni viongozi
kama sisi; hivyo wajibu wetu ni mmoja tu kuwatumikia wafanyakazi,” Dk. Shein alisema.
Rais
Shein alitoa wito kwa viongozi wa ZATUC kuendelea na mashauriano na
serikali mara kwa mara ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali
zinazowakabili wafanyakazi nchini na kuwapa taarifa mara kwa mara
wafanyakazi juu ya hatua zinazofikiwa.
“Milango iko wazi, tuendelee kushauriana mara kwa mara isiwe karibu na ‘Mei Day’ tu," alisema Dk. Shein.
"Wote lengo letu ni moja ambalo ni kuwatumikia wafanyakazi wenzetu.”
Aliutaka
uongozi wa ZATUC kuendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali na
kufuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wa makubaliano mbalimbali
yanayofikiwa wakati wa vikao vya mashauriano kati ya serikali na vyama
vya wafanyakazi.
Dk.
Shein aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali
imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma
na kuahidi kuendelea kufanya kila jitihada kulipa malimbikizo ya madeni
ya watumishi, ikiwemo malipo ya likizo.
Katika
mazungumzo hayo ZATUC lilimpongeza Dk. Shein na serikali yake kwa
kuimarisha maslahi ya watumishi na kuongeza fursa za ajira nchini.
“Tunazipongeza
jitihada zako na za serikali unayoingoza kwa kuimarisha muundo wa
utumishi wa umma na maslahi ya watumishi pamoja na kuongeza ajira
nchini” Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohamed alisema.
Alibainisha
kuwa ZATUC imefurahishwa sana na ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza
mshahara wa kima cha chini hadi kufikia Sh. 300,000.00 kwa mwezi.
“Tunashukuru
kuona kati ya mambo 12 tuliyozungumza katika kikao chetu cha tarehe 14
Aprili mwaka jana, mambo 10 yametekelezwa au yamo katika utekelezaji,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya
Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) baada ya mazungumzo ulipofika Ikulu Mjini
Zanzibar Ukiongozwa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana,
Wanawake na Watoto Mhe,Moudline Castico (wa pili kulia). Picha na Ikulu.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment